Hata hivyo, ikiwa msanii huyo ambaye kwa fikra zake anaamini ndiye mkali kuliko wachekeshaji wote Bongo japokuwa Mzee Majuto ndiye namba moja, anaweza kuwa mwerevu badala ya kuendelea kuwa mjinga.
KWA NINI MJINGA?
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford – Toleo la Pili) inamuelezea mjinga
kuwa ni mtu asiyejua kitu au jambo fulani.
Hata hivyo, mjinga hawezi kuendelea kubaki katika hali hiyo baada ya kufundishwa na kujua
maana.
HABARI KAMILI
Tukio la Mpoki hivi karibuni kuwadhalilisha watu waliofika jukwaani kukabidhi tuzo kwa
washindi katika Tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) kwenye Ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar ni ushahidi tosha kuwa ana tatizo la kufikiri.
Ukiachana na tukio hilo, rekodi yake ya maisha yake ya kisanii na nje ya sanaa inathibitisha
asivyo hodari wa kutumia ubongo wake sawasawa, vijana wa mtaani huita zero brain (0).
Kwa uelewa wake, uchekeshaji ni udhalilishaji ndiyo maana vipande vingi anavyoigiza huwa anawasema watu vibaya hata wale ambao wamemsadia kufika alipo kisanii.
TUZO ZA KILI
Katika hali ya kawaida, kwa mtu asiye mjinga na anayejitambua, Mpoki asingeweza
kumkejeli mtu mwenye heshima zake kama Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi wa Aset.
Asha anaweza kuwa mama yake lakini bila haya alimwambia mbele ya hadhara kuwa kwa
alivyo na mwonekano mzuri kwa usiku ule, asubuhi yake angeweza kusalimiwa shikamoo (akimaanisha angekuwa na mwonekano wa kizee kwa kuwa hatakuwa na make up tena).
Hakuishia hapo, Mpoki alifikia hatua ya kuingilia hadi mambo binafsi ya watu ambayo katika
hali ya kawaida hayawezi kuwa utani, alimwambia Maimartha Jesse kuwa licha ya kwamba ananyonyesha lakini amepiga matiti jeki. Upuuzi mtupu!
NJE YA KILI
Ukiachana na kero alizotoa kwenye jukwaa lile linaloheshimika, Mpoki ana tabia ya
kuwadhalilisha watu hata anapokuwa kwenye kazi zake. Mifano ipo mingi.
Kutokana na kile kinachoonekana kutojielewa, Mpoki humkejeli mtu makusudi ili
kutengeneza bifu akiamini magazeti yakimwandika ataendelea kuwa juu.
Hivi karibuni alitoa wimbo ambao ndani yake amewatukana baadhi ya watu akiwemo mwandishi mmoja mashuhuri nchini wa magazeti pendwa kwa kumuita dada wakati akijua ni mwanaume (anapenda misala).
Kwa akili zake fupi, aliamini paparazi huyo angepaniki na kurushiana naye maneno kwenye magazeti na mitandao ya kijamii, hakufanya hivyo na mpaka sasa yuko kimya kabisa kama hakuna kitu kilichotokea kwa sababu ni mwerevu.
Pia jamaa huyo bila haya wala soni aliwahi kuigiza kwa kumkejeli Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi kwenye maigizo yao ya Orijino Komedi.
Ikumbukwe kuwa, Televisheni ya Afrika Mashariki (EATV) inayomilikiwa na mzee Mengi ndiyo iliyorusha kipindi chao cha vichekesho kwa mara ya kwanza. Kifupi ndiye aliyemtoa baada ya kupigika kwa muda mrefu.
Mpoki alitambulishwa kwa mara ya kwanza na Runinga ya ITV akiwa na Kundi la Nyota Ensemble kupigtia Kipindi cha Mambo Hayo cha ITV ambacho ni mali ya mzee Mengi.
WADAU WACHARUKA
Wadau wa burudani Bongo waliopata kuzungumza na Ijumaa kwa nyakati tofauti, walionesha hisia zao za wazi kwa namna walivyokasirishwa na msanii huyo mwenye mdomo mchafu na asiyepima maneno.
Wapo waliokwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba ikiwa kutakuwa na shughuli yoyote ya kiburudani na msanii huyo akapangwa kuwa MC basi hawatahudhuria kwa kuogopa kudhalilishwa.
Nasra Abdillah wa Tabata jijini Dar alisema: “Mimi nahisi kuna kitu cha zaidi kwa Mpoki, si kwamba ni mchekeshaji, nadhani kichwani hayupo vizuri. Mimi nilikwenda Mlimani City siku ile, kuna ndugu yangu alikuwa mmoja wa watoa tuzo.
“Alipoona kila anayepanda anadhalilishwa (ingawa kwa Mpoki ni utani) akaingiwa hofu. Ilifika mahali akatamani kuahirisha kwenda kutoa tuzo, tukampa moyo lakini alipopanda mambo yakawa yaleyale, akadhalilishwa waziwazi.
“Mpoki anatakiwa kubadilika. Nampa ushauri wa bure, ajifunze kupitia kwa wengine. Lakini hata hivyo mimi popote ambapo yeye atakuwa mshereheshaji, sitakanyaga hata kwa dawa.”
Dulla wa Sinza Kwaremmy alisema: “Sikufurahishwa na kitendo cha kumwambia Dj Bon Love na wadogo zake kwamba ni wabahili wa fedha na kumshangaa Vanessa Mdee kwa kuzungumza Kiingereza wakati yeye ni Mpare azungumze Kiswahili, halafu akamkejeli eti awe anafanya mazoezi ya kuvaa viatu virefu baada ya kunusurika kuanguka jukwaani. Ule si utani ni udhalilishaji.”
Mdau mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema: “Sikufurahishwa kabisa alivyomwambia Isha Mashauzi, eti ni mwanamke wa Kikurya, si wa kuoa.
Lakini mbaya zaidi akamwambia make up zilimfanya aonekane msichana mrembo, lakini akiamka asubuhi atapewa shikamoo kwa mwonekano mpya atakaokuwanao. Ile ilikuwa too much. Kifupi Mpoki ni mpuuzi sana.”
HUYU AWAKUMBUKA TAJI, MILLARD NA PENNY
January Kingamkono wa Msasani Dar, yeye alikwenda mbali zaidi na kuwakumbuka washereheshaji wa siku zote katika hafla hiyo, Taji Liundi, Millard Ayo, Jokate Mwegelo, Penniel Mungilwa ‘Penny’ na wengineo.
Hapa anafafanua: “Kili walichemsha kwa kweli. Kumkaribisha Mpoki lilikuwa wazo zuri lakini mizaha yake ilikuwa ya kijinga sana. Alikuwa akiwatusi na kuwakejeli watu na si kuchekesha. Nawashauri Kili wafikirie kuwarudisha akina Taji na wengine waliokuwa wakifanya vizuri kwa pamoja kama kweli wanataka hafla yao iwe na msisimko.
“Wakumbuke Tuzo za Kili siyo free event (onesho la bure), watu wanatoa pesa zao. Sasa lazima wazingatie kuwa kinachotolewa kwa watazamaji kinalingana na hela iliyolipwa. Kifupi Mpoki aliboa,” alisema Kingamkono.
HUYU ATAKA AOMBE RADHI
Mdau mwingine, Juma Alii wa Manzese ya Tip Top jijini Dar alisema: “Mpoki anatakiwa kujifunza. Kila kona sasa hivi gumzo ni yeye. Nasikia wale mastaa waliokejeliwa wanataka kumfungulia kesi, ni vyema ajifunze kusoma alama za nyakati. Ajue alikosea na aombe radhi.
“Lakini pia ni vizuri kama atajifunza kutoka kwa washereheshaji wengine, namna wanavyofanya kazi kwenye matukio rasmi kama hayo.”
TAJI ASHAURI
Mkongwe katika tasnia ya utangazaji Bongo, Taji Liundi aliona kasoro za Mpoki. Hata hivyo, kwa kutumia busara alitupia katika ukurasa wake ndani ya Mtandao wa Kijamii wa Facebook akizungumzia hafla hiyo ambapo aliandika: “Nadhani ingekuwa vema kutambulisha wasoma tuzo vizuri.
Kuna mtu mmoja “Mhaya Mweupe” angestahili kuwasilisha kwa umakini zaidi!! Pia tunasikia mazungumzo ya watangazaji na watu nyuma ya jukwaa kupitia mic zisizozimwa. Onesho lina msisimko lakini nadhani “production” imekuwa na changamoto!
Maneno hayo yalitupiwa na Taji, Mei 4, mwaka huu muda mfupi tu wadau wakaibuka na kulipuka. Wa kwanza alikuwa ni Dinne Shose ambaye aliandika:
“Yaani Taji nimeliwaza hilo nikawa nawaambia wadogo zangu...imekuwaje? Wapi Taji?...ma MC hawana mvuto...utani upo lakini hauchangamshi matokeo yake utani umezidi hadi unaboa watu...wish Taji, Millard, Jokate na Penniel mngekuwa ma MC.”
Mara moja, Taji akajibu: “Dinne ahsante kwa maoni. Sisi wazoefu tutapata majukwaa mengine. Nadhani Shadee kajitahidi sana lakini shoo ilikuwa ndefu, focus inaweza kupotea. Mpoki katumia mtindo wa Kevin Hart akiwa ana-MC BET.”
TAJI AMTOLEA UVIVU
Baada ya mjadala kuwa mkali huku wachangiaji wengi wakipeleka lawama zao moja kwa moja kwa Mpoki, Taji aliamua kumtolea uvivu kwa kuandika hisia zake kwa ukweli kuhusu ubovu wa aliouita utani lakini kumbe ni udhalilishaji.
Sehemu ya maandishi ya Taji yanasomeka: “Hakuna shaka kwamba Mpoki ni mchekeshaji mzuri. Hapo juu nimeelezea mtindo wake wa kukejeli alipoutoa. Ni kwa mchekeshaji mwenzake Kevin Hart. Je, alipitiliza? Nadhani NDIYO. Kwa Bon Luv na Ray Kigosi. Sikumwelewa Mpoki. Nadhani Martin Kadinda naye hakupendezwa.
“Hapo sasa kuna tofauti ya KUCHEKESHA na KUBEZA, pia ya kuwa MC! Kasoro nyingine niliyoiona ni kurusha watu, Fina, Ruge... Sijui kama ilikuwa kwenye script. Mchango wa Fina unaeleweka kupitia OnePlus (kejeli za Mngoni kuzaa na Mzungu hazikuwa na ladha).
“Naamini Mpoki atapokea maoni chanya ili aweze kuji-balance akifungua mdomo. Ajipange. Kuna kitu kinaitwa MANENO MATUPU, kama vile kujitangaza kuwa ni MC wa harusi angali anafanya KTMA mara ya pili na kuaminika, masuala ya kulipwa ontime mbele ya Kavishe???? Matani ya “kiutu uzima” kwenye Live TV, watoto wanaangalia!!
“Anyway, yote haya hayatakosa kukosolewa kwa tamasha kubwa kama lile. Nadhani hakuna mchangiaji anayechukia KTMA. Kuomba ushauri wasiache.
Ikiwa watu wanalewa ukumbini, unategemea nini kama nusu ukumbi ukiamka kumtuza, kumtukana Diamond au kuwafuata wasanii backstage? Dah!! Kungekuwa na bucket la maji kwa kila mchemshaji! Ni kusema lile tangazo nalo tata! Si Sprite vile? Naona kama watu watamwagiana pombe??!”
MDAU MWINGINE
Edwine Ndaki alisema: “ Taji Liundi upo sahihi, nimependa ulifanya uchambuzi na ushauri.
Kwa sisi tulio nje ya nchi tunapongeza kwa wazo la kurusha event live online.
Mpoki next time au popote inabidi aangalie utani gani na wapi.”
JIMMY CHOCOLATE MKATTE
“Iko haja ya ma - MC kufanyiwa rotation, rafiki yangu
Mpoki alibweteka akamnyima Co - MC nafasi. That was illegal.”
BINTI SHANGWE
“Kasoro kibao, MC wameboa, hakuna mpangilio, huyu hajamaliza kuongea,
huyu kashadakia, hasa Mwarabu wa Dubai, mtu anayetaja jina la mshindi na
MC inabidi wapokezane mic...”
KILI: HATUKUJUA KAMA ANGEHARIBU
Mmoja wa wanakamati ya maandalizi ya tuzo hizo, kwa sharti la kutotajwa jina lake
gazetini kwa maelezo kuwa si msemaji, alizungumzia kuhusu udhalilishaji
uliofanywa na Mpoki, akasema hawakujua kama angefanya vile.
“Tulimwamini maana tulishawahi kufanya naye kazi. Kilichotokea pale
kilitushangaza sana lakini isingekuwa rahisi kumrekebisha wakati akiwa tayari
yuko jukwaani. Pengine utekelezaji wa hilo ungesababisha tatizo jingine kubwa zaidi.
Niseme tu, tumejifunza.”
KUTOKA DAWATI LA IJUMAA
Mpoki, wewe ni staa na una heshima kubwa kwenye jamii. Kila binadamu amepewa akili;
uwezo wa kufikiri upo kwa kila mmoja tatizo ni pale kwenye uamuzi wa kutumia.
Ni vyema sasa ukabadilisha staili ya maisha na uanze kutumia akili yako ipasavyo.
Vichekesho siyo kuwadhalilisha watu, lakini kubwa zaidi kumbuka ulipotoka,
acha kuwakejeli hadi waliokusaidia – hata hivyo si uungwana kuwadhalilisha watu.
Badilika ili uondoke kwenye ujinga kwa kuchekesha vitu vyenye mantiki ili uwe mwerevu. Inawezekana ukiamua! – MHARIRI.
Post a Comment