>>TFF, PLAN INTERNATIONAL KUHAMASISHA HAKI ZA MTOTO
>>KOZI YA UKOCHA LESENI B YAFIKIA TAMATI
SOMA ZAIDI:
Release No. 109
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Juni 19, 2014
TFF, PLAN INTERNATIONAL KUHAMASISHA HAKI ZA MTOTO
Wakati
mamilioni ya Watanzania wakifuatilia Fainali za Kombe la Dunia nchini
Brazil, Shirika la kutetea haki za watoto la Plan International
limeingia ubia na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili
ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.
Kwa lengo hilo, mkataba wa ushirikiano
umesainiwa leo katika ofisi za makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam
baina ya Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen na
Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Ushirikiano huo unalenga kufanya kazi pamoja
katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za
utotoni.
Kwa mujibu wa Haldorsen, mchezo wa mpira
ndio unaoongoza nchini na kote duniani kwa kuwa na ushabiki mkubwa na
kwamba joto kali juu ya Fainali za Kombe la Dunia linaloendelea Brazil
ni ushahidi tosha.
“Tunatambua uwezo wa mchezo huu wa
kuwajumuisha watu. Sasa tunataka tuwajumuishe watu sio tu kwa ajili ya
furaha lakini pia kama njia ya kuleta mabadiliko juu ya usawa wa
kijinsia kwa kutetea na kuhamasisha juu ya haki za mtoto wa kike,”
aliongeza.
Mkurugenzi huyo alidokeza kuwa
ushirikiano na TFF ni sehemu ya kampeni ya kimataifa inayoendeshwa na
shirika hilo kote ulimwenguni inayoitwa ‘Because I Am A Girl’-BIAAG au
kwa Kiswahili- KWA SABABU MIMI NI MSICHANA ambayo inalenga kuwatoa
mamilioni ya wasichana kutoka katika umaskini kupitia uhamasishaji juu
ya haki zao, elimu na stadi za maisha.
“Kwa kupitia ubia huu tutakuwa na uwezo
wa kuwafikia mamilioni ya Watanzania na tutawapa wasichana ujumbe kuwa
KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima nipate fursa sawa na wavulana. KWA
SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima niwe na uwezo wa kufunga magoli ya
kufikia ndoto zangu katika maisha,” Haldorsen alieleza.
Kwa upande wake, Rais wa TFF, ambaye ni
mjumbe katika Kamati ya Huduma kwa Jamii ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Ulimwenguni- FIFA, alisema kuwa ubia huo ni sehemu ya utekelezaji
wa sera za huduma kwa jamii ya TFF na kwamba wana furaha kushirikiana na
Plan International kwa lengo hili muhimu.
“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu
kwani unakileta chombo kikubwa kabisa cha michezo hapa nchini pamoja na
shirika la Plan International hususan kwa ajili ya haki za mtoto wa
kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu nchi nzima kuelimisha juu ya
usawa wa kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto wa kike,” alisema
Rais Malinzi.
Kwa pamoja tutashughulikia masuala ya
usawa wa kijinsia, hususan kupambana na ndoa za utotoni ambazo
zinawazuia mamilioni ya watoto wa kike nchini wasiweze kumaliza shule,
kufikia ndoto zao katika maisha, na vile vile kuwaacha waendelee
kuteseka katika umaskini,” Rais Malinzi aliongeza.
KUHUSU PLAN INTERNATIONAL: Plan
International ni shirika la kimaendeleo la misaada ya kibinadamu,
linalomlenga mtoto lisilofungamana na mrengo wowote wa kidini, kisiasa
au kiserikali.
Plan International ilianzishwa zaidi ya
miaka 70 iliyopita na inaendesha shughuli zake katika nchi 70 duniani.
Plan International imekuwa inafanyakazi hapa Tanzania tangu mwaka 1991
ikiwasaidia watoto na jamii kupata huduma za afya, elimu, maji, usafi na
mazingira, kujikimu na ulinzi. Inaendesha miradi Dar es Salaam,
Morogoro, Dodoma, Geita, Pwani, Mwanza na Rukwa.
KAMPENI YA KWA SABABU MIMI NI MSICHANA –BIAAG: Kampeni
ya Kwa Sababu Mimi ni Msichana-BIAAG (2012-2016) ni kampeni ya Plan
ulimwenguni kote inayolenga kuelimisha na kutetea haki za mtoto wa kike
na kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka kwenye lindi la umaskini
kupitia elimu na utoaji wa stadi za maisha na kazi.
Kampeni hii inalenga kupambana na
ubaguzi wa kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana milioni 4 duniani
na zaidi ya laki 3 hapa Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga shuleni,
kupata stadi za kiufundi na maisha, kujikimu, na kushiriki katika
shughuli mbalimbali katika jamii na kulindwa, kwa kukabiliana na vikwazo
dhidi ya maendeleo ya mtoto wa kike.
KOZI YA UKOCHA LESENI B YAFIKIA TAMATI
Kozi ya makocha wa mpira wa miguu ya
Leseni B inayotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
iliyodumu kwa wiki mbili inafungwa kesho (Juni 20 mwaka huu) jijini Dar
es Salaam.
Makocha 26 kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar wameshiriki katika kozi hiyo chini ya wakufunzi wa CAF, Sunday
Kayuni, Salum Madadi wa Tanzania na Honory Janza kutoka Zambia. Ufungaji
wa kozi hiyo unatarajiwa kufanywa saa 5 asubuhi kwenye hosteli za TFF
zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Walioshiriki kozi hiyo ni Abdalla
Mohammed Juma (Zanzibar), Abdul Banyai (Temeke), Abdul Nyumba (Temeke),
Abdulmutik Haji (Zanzibar), Aley Mohammed (Zanzibar), Ali Vuai Shein
(Zanzibar), Dennis Kitambi (Morogoro), Dismas Haonga (Ilala), Emmanuel
Massawe (Shinyanga), Fikiri Elias (Arusha), Fulgence Novatus (Mwanza),
Hababuu Ali Omar (Zanzibar), Juma Mgunda (Tanga) na Kidao Wilfred
(Ilala).
Wengine ni Maka Mwalwisi (Mbeya), Malale
Hamsini Keya (Zanzibar), Mecky Maxime (Morogoro), Mohammed Tajdin
(Temeke), Mussa Furutuni (Dodoma), Nassor Salum Mohamed (Zanzibar),
Peter Mhina (Ruvuma), Said Mohamed Abdulla (Zanzibar), Salim Makame
(Zanzibar), Salum Ali Haji (Zanzibar), Sebastian Nkoma (Ilala), Wane
Mkisi (Dar es Salaam).
26 WAITWA STARS SAFARI YA GABORONE
Wachezaji 26 wa Taifa Stars wanaingia kambini Jumatatu (Juni 23 mwaka huu) kwa ajili ya safari ya Gaborone, Botswana.
Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa timu
hiyo Salum Mayanga, wachezaji hao wanatakiwa kuripoti katika hoteli ya
Accomondia jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa safari hiyo inayotarajiwa
kuwa Juni 24 mwaka huu.
Wachezaji hao ni wanaotakiwa kuripoti
kambini ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Benedictor Tinoko, Kelvin
Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub, Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar
Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na Pato Ngonyani.
Wengine ni Frank Domayo, Amri Kiemba,
Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haruna Chanongo, Himid Mao, John
Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano, Khamis Mcha, Mrisho
Ngasa na Mwegane Yeya.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Post a Comment