Kwa muda mrefu wafuasi wa mwanamuziki Ally Salehe Kiba maarufu
Alikiba, wamekuwa wakijiuliza sababu zilizomfanya mwimbaji huyo kukaa
kando ya muziki kwa muda mrefu.
Alikiba ambaye aliachia wimbo wake wa mwisho “My
Everything” Novemba 2012 hajawahi kuachia tena wimbo mwingine, licha ya
kutoa kazi kadhaa alizokuwa akishirikishwa na mdogo wake msanii Abdu
Kiba ukiwamo “Kidela”.
Starehe ilikaa kitako na msanii huyu aliyewahi
kutamba na wimbo wake wa kwanza “Sinderela” mwaka 2007, nyumbani kwake
Kunduchi Beach na ambapo aliainisha mambo makubwa matatu yaliyomfanya
asimame kwa muda kuachia kazi za muziki.
“Kuna mambo matatu ya msingi niliyokuwa nayafanya
kwa kipindi hiki cha miaka mitatu. Awali ya yote niliamua kusimama ili
kumlea mwanangu, malezi ya mtoto yalinifanya niegemee huko hadi umri
wake usogee ndipo nirudi kwenye muziki,” anasema pasipo kufafanua vizuri
iwapo ni wa kike au wa kiume.
Anasema familia yake ni kitu chenye uthamani mkubwa kwake ndiyo maana alijitoa ili kuhakikisha inakaa sawa.
“Jambo la pili ambalo najivunia kulifanikisha kwa
kipindi hiki, ni kuweza kumsimamisha sehemu nzuri mdogo wangu Abdu Kiba
katika ramani ya muziki. Hili lilikuwa suala kubwa na nyeti kwangu
kuhakikisha anatimiza ndoto zake nilijitahidi kumpa nyenzo ili na yeye
ajulikane kwani nilimuona ana kipaji kikubwa,” anasema.
Jambo la tatu analifafanua kuwa ilimchukua muda
kufikiria namna atakavyowaacha wasanii wengine Tanzania, na wao
wajulikane ndani na nje ya nchi.
“Tatu niliona nitulize kichwa kidogo kwa kufanya
biashara na pia kuwaacha wasanii wengine na wao kipaji chao kionekane na
kuwapa nafasi ya kufanya vizuri ndani na nje ya nchi, nashukuru hilo
limefanikiwa tena kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa kwa kipindi hicho
wameibuka wengi ambao wameweza kufanya vizuri na kwa wale ambao
walikuwepo kitambo wamepanuka zaidi kifikra,” anasema Alikiba.
Anasema kwa kipindi cha miaka mitatu aliyopumzika,
amejifunza mengi na pia ameona kumekuwa na mapungufu katika tasnia ya
muziki wa kizazi kipya na maendeleo pia.
“Mapungufu yamekuwepo, lakini kuna mafanikio mengi
pia, kuna baadhi ya wasanii wamefanikiwa kufanya muziki mzuri na
kuutangaza kimataifa na wengine wametengeneza kazi nzuri, lakini
kinachonitisha ladha ya muziki wetu asili hasa ya bongofleva, imepotea
tumeanza kutengeneza muziki wenye utofauti mkubwa sana na kipindi cha
nyuma, kwa kuiga ala ya muziki wa Nigeria na mataifa mengine,” anasema
Alikiba.
Albamu mbili, singo mpya wiki ijayo
Alikiba aliyetamba na wimbo “Dushelele” miaka
miwili iliyopita, ameweka wazi ujio wake wiki ijayo akiwa chini ya
kampuni kubwa barani Afrika ambayo hajataka kuiweka wazi, anasema
alikuwa ‘chimbo’ kwa takribani miaka miwili akiandaa kazi mpya ambapo
amefanikiwa kukamilisha albamu mbili na punde kuachia singo mpya.
on Saturday, June 21, 2014
Post a Comment