************
Dar es Salaam. Tanzania imeomba msaada kwa
taasisi iitwayo International Centre for Asset Recovery – ICAR (Kituo
cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali) ya Uswisi kuchunguza kesi tano
zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha
nchini humo.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuibuka kwa sakata la
mabilioni hayo ya Uswisi, Serikali iliunda kikosi kazi chini ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kulifanyia kazi.
Gazeti hili lilifuatilia suala hilo hadi Uswisi na
kubaini kuanza kwa uchunguzi huo, huku fedha nyingi zikitajwa kwamba
zinatokana na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na mwandishi wetu mjini Bern, Uswisi
hivi karibuni, Mtafiti wa Sheria wa ICAR, Andrew Dornbierer alisema:
“Tuna makubaliano na Serikali ya Tanzania hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), tunachunguza kwa kina kesi za rushwa na utoroshwaji
wa fedha, hivyo tuko katika ukusanyaji wa taarifa. Siwezi kukupa mifano
ya moja kwa moja kwa sababu bado tunazifanyia kazi na tunadhibitiwa
katika utoaji wa taarifa.”
Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Fenner Zinkernagel alithibitisha uwepo wa kesi hizo za Tanzania.
“Ni kweli tumeombwa na Serikali ya Tanzania
kusaidia kuchunguza baadhi ya kesi… zilikuwa zimeshachunguzwa lakini
kutokana na uwezo wao mdogo tunawasaidia. Kwa harakaharaka naweza kusema
tunazo kesi tano hivi… ni kesi za watu binafsi na taasisi na zinahusu
masuala ya fedha. Hatuwezi kutaja majina kwa sababu tunakatazwa kabisa
na mkataba wetu na taasisi tunazofanya nazo kazi.”
Licha ya kutotaja majina, Zinkernagel alisema
wanaochunguzwa katika kesi hizo wanahusishwa na kampuni hewa
zilizoanzishwa kwa lengo la kuchota fedha kisha kwenda kuzificha nje ya
nchi.
“Kuna watu wenye masilahi binafsi na wamekuwa
wakipokea rushwa au wamekuwa wakitumia mashirika kwa ubia au kampuni
kivuli na ushirika mwingine wa kimataifa ili kusafirisha fedha kwenda
kwenye kampuni fulani kwa lengo la kuzificha. Ni kampuni zinazotumiwa na
wafanyabiashara kuhamisha fedha haramu na mwisho hujisafisha,” alisema.
Jaji Werema
Jaji Werema alikiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya
uchunguzi huo lakini akakataa katakata kutaja watu wala kampuni
zinazofanyiwa uchunguzi.
“Hatuwezi kutaja majina ya watu waliofunguliwa
kesi kwa sababu kwanza tutakuwa tumeingilia haki zao kisheria. Pili,
tunaweza kuwataja lakini baadaye ikabainika kuwa si kweli, bali ni
tuhuma tu na wakaja kutushtaki na tatu, tutakapowataja watu hao
tuliowafungulia kesi tutaharibu upelelezi wetu.
“Katika kesi hizi, kisheria, tunafanya kazi zetu
kwa utaratibu ili tusiharibu upelelezi na tupate mambo mengi. Mnadhani
tumekaa kimya hatufuatilii lakini tunafanya kazi yetu. Siku ikifika
mtaona na mtasikia.”
Post a Comment