Kijana
Amos Ng’arare Sasi mwenye umri wa miaka 21, mkazi wa Kijiji cha Kizaru,
Kata ya Mryaza, Musoma vijijni anyesumbuliwa na uvimbe.
Kwa karibu miaka 17 sasa, kijana Amos
Ng’arare Sasi mwenye umri wa miaka 21, mkazi wa Kijiji cha Kizaru, Kata
ya Mryaza, Musoma vijijni anataabika kwa ugonjwa ambao umempeleka katika
hospitali nyingi bila mafanikio.
Kama angeendelea na masomo yake
vizuri, hivi sasa Amosi angekuwa kidato cha nne, lakini alilazimika
kukaa nyumbani na kuwaacha wenzake wakiendelea na masomo katika Shule ya
Sekondari ya Bumangi kutokana na uvimbe kuzidi kukua.
Kwa sasa yupo katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili anakotibiwa. Akizungumza na mwandishi wa habari hii
alikuwa na mengi ya kusimulia:
“Ninaumia sana moyoni niwaonapo
wanafunzi wenzangu niliosoma nao darasa moja wakiendelea na masomo
wakati miye nakabiliana na gonjwa hili la ajabu ambalo limezima ndoto
zangu juu ya elimu, sitegemei kurudi tena darasani, nilizaliwa nikiwa
sina tatizo kiafya, nililelewa na wazazi wangu wote wawili, nikawa
naishi vizuri kama watoto wenzangu.
Kijana Amos Ng’arare Sasi akiendelea kuugua kwa uvimbe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Tatizo lilianza kama kaupele hivi nikiwa
na umri wa miaka minne, kidogo kidogo kikawa kinakua, lakini bahati
mbaya baba alifariki na mama akabeba mzigo wa kunihudumia kwa matibabu,
licha ya kipato chake kidogo kwani alitegemea kilimo, tena cha jembe la
mkono.
“Pamoja na mama kunipeleka hospitali
mbalimbali, nilikuwa napewa asprini tu kwa ajili ya kutuliza maumivu
kwani walishindwa kunipa dawa za aina nyingine kutokana na ugonjwa wangu
kutofahamika.
“Mama anahangaika na mimi hadi namuonea
huruma, kaka yangu mkubwa alitoweka nyumbani tangu mwaka 1998 akisema
anaenda kutafuta kazi, mpaka sasa hajulikani alipo na wala hajawahi
kurudi nyumbani, hali ilizidi kuwa mbaya nilipofikisha umri wa miaka
tisa, maumivu na uvimbe ukazidi.
“Mama alikuwa hapati usingizi aliponiona
nahangaika, alinipeleka hospitali ya Musoma haikusaidia, mwaka 2010
nilipelekwa Bugando kufanyiwa uchunguzi, ugonjwa haukujulikana, wakati
huo ndiyo nilikuwa nikianza kidato cha kwanza, nilienda siku chache.
“Nilirudishwa nyumbani, baadhi ya watu
wakawa hawataki kuniona mitaani, wakaniona kama vile nimeleta nuksi
katika ukoo, nikawa najificha ndani.
“Baadhi ya wananchi walinionea huruma
walinichangishia fedha ili nije Muhimbili, mara ya kwanza nilifika hapa
Septemba 2011, nikachukuliwa vipimo na kuambiwa nirudi nyumbani hadi
Desemba.
“Hata hivyo, sikuweza kurudi kipindi hicho
kutokana na kukosa nauli, baadaye nikafanikiwa kwenda nyumbani. Tatizo
likawa namna ya kufuata majibu, lakini baadaye nilipata.
“Mara ya pili nilikuja Februari mwaka huu
kwa msaada wa nauli kutoka kwa diwani wetu pamoja na Mbunge Nimrodi
Mkono, walinipima kwa mara ya pili na kunieleza kuwa kuna mshipa wa
fahamu unapitisha damu nyingi hivyo natakiwa kufanyiwa upasuaji nchini
India.
“Kuna kipindi napata maumivu hadi napoteza
fahamu, uvimbe unazidi kufunika macho, sioni vizuri, madaktari wapo
karibu na mimi, wananipa dawa za kupunguza maumivu, wananisaidia sana,
ninawashukuru, lakini naumia zaidi ninapowaona wagonjwa wenzangu
wakitembelewa na ndugu zao, mimi sina mtu hata mmoja.
“Ninaomba Watanzania wenzangu wanisaidie,
japo kwa maombi ili niweze kupata msaada wa kwenda India kwa matibabu,
napenda nipone, nirudi nyumbani kumuona mama.”
Kwa walioguswa na simulizi ya kusikitisha
ya Amos wanaweza kumsaidia ushauri au fedha kupitia simu zake za
kiganjani ambazo ni 0765 765747 na 0715 756384.
Post a Comment