Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ameonja chungu
ya uamuzi wa Serikali wa kusitisha mikutano ya hadhara katika mikoa ya
Lindi na Mtwara baada ya kushindwa kufungua mashina ya chama hicho mjini
Mtwara.
Nape ambaye alikuwa mkoani Mtwara kwa ziara ya
siku moja, alijikuta akiishia kuwakabidhi bendera za chama hicho
viongozi wa matawi ili wakazipandishe wenyewe kimyakimya.
Akizungumzia hatua hiyo, Nape alisema amri hiyo ya
kusitisha mikutano imekuwa kikwazo na inadidimiza demokrasia katika
mikoa hiyo, hivyo Serikali inapaswa kuibadili ili kuruhusu iendelee
kufanyika. Mashina ya chama hicho ambayo yalitarajiwa kufunguliwa
mwishoni mwa wiki ni Shapriya, Coco Beach na Kwajionee.
“Ni kweli ilikuwa twende kuzindua kwenye maeneo
yenu lakini… lipo agizo ambalo lilitolewa na Serikali kuzuia mikutano
katika mikoa hii, kupitia kwenu ipo haja ya kufungua mikutano ili
demokrasia ipanuke zaidi,” alisema Nape na kuongeza:
“Amri hii kwa mtazamo wangu inabaka demokrasia,
lazima mikutano iruhusiwe kama hali ni mbaya, kazi ya Serikali ni
kulinda huo usalama… nitakwenda kushauriana nao ili mikutano ifunguliwe,
sidhani kama masikio yanaweza kuzidi kichwa.”
Akizungumzia hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Maisha Maganga alisema Serikali haijatengua agizo hilo.
Credit: Mwananchi.
Credit: Mwananchi.
Post a Comment