MBUNGE wa
Ubungo, John Mnyika, anakusudia kumshitaki Waziri wa Maji, Profesa
Jumanne Maghembe, kwa madai ya kumnyima nyaraka zinazohusiana na miradi
ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mnyika
amesema kuwa anataka mahakama imlazimishe Waziri Maghembe, azitoe
nyaraka hizo ili mbunge huyo azifanyie kazi anayokusudia.
Akizungumza
na Tanzania Daima, wakili wa Mnyika, John Mallya, alisema amepokea
maelekezo kutoka kwa mbunge huyo kufungua kesi hiyo.
Alibainisha kuwa Mnyika anataka nyaraka hizo zimsaidie kuwakilisha wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali.
Kwa
mujibu wa wakili, wengine watakaojumuishwa katika kesi hiyo ni pamoja na
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), Fredrick Werema.
Wakili
Mallya, alisema mteja wake aliomba nyaraka hizo na kwa mujibu wa kifungu
cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, alishafuata
taratibu zote husika, lakini Waziri Maghembe hakumpa nyaraka hizo.
Mallya,
alisema Mnyika alishamuandikia barua Prof. Maghembe, kuomba nyaraka hizo
tangu Januari 3 mwaka 2013 kisha kumkumbusha tena Mei mwaka huu, lakini
hatoi majibu.
Mnyika
pia anataka mikataba yote ya maji inayotekelezwa katika jimbo la Ubungo
ikiwa pamoja na fedha za mikopo ya ndani na nje pamoja na ripoti za
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali za mwaka 2010 hadi 2013,
zilizokaguliwa.
Januari
mwaka huu, mbunge huyo alimtaka Prof. Maghembe ajiuzulu kutokana na
kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam
kinyume na maelezo yake aliyoyatoa bungeni Februari 4 mwaka jana.
CREDIT:MTANZANIA DAIMA
Post a Comment