Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamemuua kinyama kwa kupiga
risasi moja ya kichwani mwenyekiti wa chama cha mapinduzi kata ya
Busambala wilayani Butiama mkoani Mara Bw Willison Opio mwenye umri wa
miaka 60 huku kichwa chake kikisambaratishwa kabisa na risasi hiyo.
Mauaji
hayo ya kinyama yamefanyika saa saba usiku wa kuamkia jana,baada ya
majambazi hayo kuvunja milango ya nyumba aliyokuwa amelala
kiongozi huyo na familia yake katika kijiji cha Kwikuba kabla ya
kumshambulia kwa bapa za panga mke wamarehemu Bi Agness Wambura ambaye
alilazimika kuwapa kiasi cha shilingi laki nne ambazo alizikopa
kutoka katika taasisi moja ya fedha.
Afisa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Mara ACP Rogati
Mlashan,akizungumza toka eneo la tukio, amesema baada ya
majambazi hayo kuvunja milango miwili ya nyumba hiyo, walipiga risasi
tatu na moja kumpata kichwani kiongozi huyo wa CCM na kufariki dunia
papo hapo na kusema kuwa jeshi la polisi litafanya kila liwezavyo
ili kuhakikisha wote walihusika kufanya uhalifu huo wanakamatwa na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa serikali katika kata ya
Busambala,wakizungumzia tukio hilo pamoja na kuonyesha masikitiko yao
baada ya kupata taarifa za kifo cha kiongozi huyo wa CCM,wameliomba
jeshi la polisi kuendesha msako mkali ambao utawezesha kukamatwa kwa
wahusika,hatua ambayo wamesema itasaidia kuondolea wananchi hofu kubwa
waliyonayo sasa.
Post a Comment