IKIWA
zimebaki siku 10 kufungwa kwa shughuli ya kupokea maombi ya mikopo ya
elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2014/2015, takribani wanafunzi 39,000
wameshatuma maombi yao kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB).
Akizungumza
jana kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kwenye
viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na
Mawasiliano (HESLB), Cosmas Mwaisobwa alisema idadi hiyo ni kwa
wanafunzi wapya pekee.(Martha Magessa)
HESLB
ilifungua dirisha la kutuma maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2014,
Aprili mwaka huu na maombi hayo yamekuwa yakifanywa kwa njia ya mtandao
(OLAS) na yatafungwa Juni 30.
Serikali
imetenga kiasi cha Sh bilioni 306 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi
98,000 wa vyuo vya elimu ya juu nchini, ikiwa wanafunzi wapya na
wanaoendelea na masomo.
“Wanafunzi
wanaotaka kutuma maombi yao ni vyema wakatumia muda huu uliobaki, kwani
Bodi haitatoa muda wa nyongeza kwa watakaochelewa kutuma maombi yao,”
alisema.
Akizungumzia
hatua ya Bodi kufungua ofisi ya Kanda ya Ziwa, mkoani Mwanza, Mwaisobwa
alisema hii ni katika kutekeleza mikakati ya Bodi katika kusogeza
huduma karibu na wananchi.
“Mpango
mkakati wetu wa miaka mitano kuanzia mwaka 2010, ilikuwa ni kufungua
ofisi za kanda katika kuongeza ufanisi katika kuwahudumia na kusogeza
huduma kwa wananchi, na mpaka sasa tumefungua ofisi za kanda tatu.”
Mbali na
ofisi ya Mwanza itakayohudumia mikoa sita ya Simuyu, Geita, Shinyanga,
Kagera, Mara na Mwanza yenye, pia Bodi ina ofisi katika Kanda ya Kati
yenye ofisi Dodoma na Zanzibar.
Alisema
ofisi ya Mwanza itakuwa inafanya majukumu yote ikiwamo ya utoaji mikopo
kwa wanafunzi wenye sifa waliodahiliwa na urejeshwaji wa mikopo kwa
wanufaika wa mikopo hiyo.
“ Ofisi
hii itasaidia sana wananchi ambao walikuwa wakilazimika kutumia siku
nyingi kufika ofisi zetu Dar es Salaam kupata huduma, lakini sasa
watahudumiwa huko huko,” alisema.
CHANZO:HABARILEO
Post a Comment