Kufuatia
umeme kukatika ndani ya bunge wakati wa kupiga kura za kupitisha bajeti
kuu ya serikali 2014/2015, hali hiyo imelikwaza bunge na kulazimu spika
Anna Makinda kumtaka waziri wa nishati na madini kueleza sababu za
tatizo hilo.
Akizungumzia
suala hilo bungeni Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
ameanza kwa kuomba radhi na kudai kuwa umeme haukukatika bungeni pekee
bali umekatika nchi nzima.
Prof
Muhongo amesema sababu ya kukatika umeme ni mitambo ya kufua umeme
inayotumia maji, mafuta na gesi imechoka ghafla na kwa mpigo hali
iliyosababisha umeme kukatika kwa zaidi ya nusu saa.
Aidha
waziri huyo ameiagiza Tanesco kuomba radhi watanzania kwa tatizo hilo
na kutoa maelezo ya kitaalamu ya kwa nini umeme umekatika nchi nzima
haraka iwezekanavyo.
Kukatika huko kwa umeme hii leo kumepelekea kukwama kwa zoezi la kupiga kura bungeni ili kupitisha bajeti kuu ya serikali.
hata
hivyo zoezi la kupiga kura limekamilika baada ya umeme kurudi ambapo
wabunge 300 wamepiga kura, kati yao 234 wamesema ndiyo bajeti ipite na
66 wamesema hapana isipite, hivyo bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha
2014/2015 kupitishwa.
Na Edwin Moshi
Post a Comment