Jaji
mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Mwanza Mh. Aishiel Sumari amewataka
wananchi kujenga tabia ya kuandika wosia ili kulinda haki ya warithi
baada ya kifo, jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza
migogoro ya kugombea mali na maiti, sanjari na kuwalinda watoto wa nje
ya ndoa ambao kisheria hawapaswi kurithi mali iliyoachwa na marehemu.
Jaji huyo mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Mwanza ametoa
changamoto hiyo jijini Mwanza wakati akifungua kongamano lililoandaliwa
na shirika la msaada wa sheria Mwanza, lenye maudhui yasemayo, ‘ linda
haki za uwapendao, andika wosia ambapo amesema katika jamii nyingi
duniani, wosia ni kitu kinachotambulika kutokana na kuwa na nguvu za
kisheria ambapo kwa hapa nchini sheria za mirathi zinatambua kuwepo kwa
wosia, ulioandaliwa na mwenye kumiliki mali wakati akiwa bado yu hai na
vilevile akili zake zikiwa bado timamu.
Mapema mkurugenzi mtendaji wa shirika la msaada wa sheria Mwanza
Bw. Heri Emanuel amesema kwa hali ya kawaida mtu akifariki bila kuacha
wosia sheria inalazimu vikao vya wanandugu kuketi na kuteua msimamizi wa
mirathi, jambo ambalo wakati mwingine linaweza kusababisha kutoelewana
huku gharama kubwa zikitumika katika uratibu na uendeshaji wa vikao
hivyo kama chakula, vinywaji na mifugo aliyoacha marehemu badala ya
kutumika kwa mustakabali wa warithi wa marehemu.
Mtu anapofariki bila ya kuacha wosia, waathirika wakubwa ni wajane
pamoja na watoto walioachwa na marehemu ambapo matokeo yake ni kunyimwa
haki ya kurithi, kudhulumiwa au kudhulumiana kati ya warithi na kwa hali
hiyo wananchi wanapaswa kuachana na dhana potofu kwamba kuandika wosia
ni uchuro na njia pekee ya kuepusha migongano ya aina hiyo ni mtu
kuandika wosia kuliko ule wa kutoa kwa mdomo.
Post a Comment