Leo
ndio siku ya mwisho kwa wabunge kujadili hotuba ya bajeti ya Waziri
Saada na kesho Waziri ataanza kujibu hoja akishirikiana na Naibu wake,
Mwigulu Nchemba na Adam Malima.
Katika
majibu yake, Waziri Saada anatarajiwa kuonesha namna Serikali
ilivyojipanga kusimamia nidhamu ya makusanyo na matumizi ya fedha za
Serikali, ikiwemo hatua aliyoitangaza ya kufuta misamaha ya kodi isiyo
na tija.
Wabunge
wengi, pamoja na kuipa Serikali changamoto, walielezea kuridhika na
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika majimbo yao, hasa miradi ya
umeme vijijini na maji.
Pia
ufikishaji wa bomba la gesi Dar es Salaam ni moja ya miradi inayoipa
Serikali sifa kwa kuwa matarajio ni Serikali kuacha kutumia fedha nyingi
katika ununuzi wa mafuta ya dizeli na petroli kwa ajili ya uzalishaji
umeme.
Aidha,
bei ya nishati hiyo kutoka kwa kampuni zinazofua umeme, inatarajiwa
kushuka kutoka senti za Marekani 30 na 60 kwa uniti moja mpaka chini ya
senti 18 za Marekani kwa uniti moja na kusaidia Serikali kutekeleza nia
yake ya kushusha bei ya umeme.
Nafuu
hiyo ya bei ya umeme, mbali na kuleta nafuu ya maisha kwa mwananchi
mmoja mmoja mijini mpaka vijijini, inatafsiriwa kuwa kivutio cha
uwekezaji, kitakachochangia ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi wa
nchi ambao kwa sasa ni asilimia saba.
Katika
mijadala ya wabunge, wengi walipongeza hotuba ya Bajeti na kutaka maoni
ya Kamati ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge (CCM), yazingatiwe kuboresha upatikanaji wa mapato.
Katika
maoni ya Kamati hiyo, Chenge alisema upo udhaifu wa Serikali katika
utekelezaji wa bajeti, kutokana na kuendelea kutegemea vyanzo vile vile
vya mapato, huku matumizi yake yakiwa makubwa ikilinganishwa na mapato.
Akiwasilisha
taarifa yake, Chenge alisema kamati yake imeshitushwa na ukuaji wa deni
la taifa, akisema ilo ni mzigo mkubwa. Alisema hivi sasa deni hilo ni
tishio kwa uchumi wa taifa.
“Serikali
imeendelea kuja na vyanzo vile vile vya kiutamaduni vilivyozoeleka,
ambavyo ni pombe, sigara, vinywaji baridi na vinywaji vikali, wakati
kuna vyanzo vingine vingi,” alisema Chenge.
Alitaja
baadhi ya vyanzo vipya ambavyo Kamati yake inaamini vinaweza kuingizia
Serikali mapato mengi, ni pamoja na uvuvi wa Bahari Kuu, kupiga mnada
vitalu vya misitu na uwindaji wa kitalii, kupiga mnada masafa ya
mawasiliano pamoja na kodi za majengo.
Kwa
mujibu wa Chenge, Kamati yake inashangazwa na majibu yanayotolewa na
Serikali kuhusu suala la ukusanyaji wa mapato katika uvuvi wa Bahari
Kuu, kwamba haiwezi kukusanya hadi itakapojenga bandari maalumu ya
uvuvi.
“Kwa
taarifa rasmi za Serikali zilizotolewa bungeni, Serikali inapoteza
takriban Dola za Marekani milioni 222, sawa na Sh bilioni 372.9. Kamati
inahoji hadi hapo tutakapojenga bandari maalumu ya uvuvi, tutakuwa
tumepoteza mapato kiasi gani,” alihoji.
Alisema
Kamati yake imechambua bajeti ya mwaka 2013/2014 na kubaini kuwapo kwa
madeni makubwa katika baadhi ya wizara na taasisi mbalimbali za umma.
“Mfano
Wizara ya Ujenzi imekuwa ikitekeleza miradi ya ujenzi wa barabara bila
kuwalipa makandarasi kwa wakati na kwa kuzingatia mikataba yao na hivyo
kujikuta ikianza kila mwaka wa fedha ikiwa na malimbikizo makubwa ya
madeni.
“Hali
hii imesababisha Wizara hii kutumia bajeti yake ya mwaka unaofuata
kulipia madeni ya mwaka uliopita, badala ya kutekeleza miradi
iliyoidhinishwa kwa mwaka husika wa fedha,” alisema Chenge.
Akizungumza
kuhusu deni la taifa, Chenge alisema licha ya Serikali kusema deni hilo
ni himilivu, lakini kwa uhalisia deni hilo ni mzigo mkubwa kwa taifa
linaloathiri uchumi wa nchi.
“Hadi
kufikia Machi 2014, deni la taifa linalojumuisha deni la Serikali na
deni la nje la sekta binafsi lilifikia Sh trilioni 30, ikilinganishwa na
Sh trilioni 23 mwezi Machi, 2013,” alisema.
Chenge alitoa sababu kadhaa zinazoifanya Kamati yake ishindwe kukubaliana na hoja ya Serikali kwamba deni hilo ni himilivu.
“Mosi,
kuna madai mengi ya ndani ambayo hayajajumuishwa katika deni la taifa
na taarifa zilizopo zinaonesha kuwa madai haya yanaendelea kuongezeka.
"Sababu
nyingine ni kwamba, uwiano uliopo wa deni la taifa na pato la Taifa
kiuchumi si wa kuridhisha, ukubwa wa deni hili hauwiani na kiwango cha
uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa sasa wa asilimia saba.
"Pia
alisema, udhaifu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na
ucheleweshaji wa uhakiki wa madai ya ndani ni sababu nyingine. Taarifa
ya Waziri wa Fedha ya nusu mwaka inaonesha, malimbikizo ya madai hadi
Desemba, 2013 yalikuwa yamefikia Sh trilioni 2.09, ambayo ni asilimia
nne ya pato la Taifa,” alisema.
Wabunge
wengi pia walisema punguzo la Kodi katika Mshahara (Paye), kutoka
asilimia 13 mwaka unaoisha wa fedha 2013/2014 mpaka asilimia 12 kwa
mwaka ujao wa fedha 2014/2015, kuwa ni ndogo.
Post a Comment