Mwanafunzi
Norat Rashid akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya
Fahamu (MOI) iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
MATESO
ya mwanafunzi Norat Rashid (16), anayesoma kidato cha pili katika Shule
ya Sekondari Mtoni Relini, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam ni ya
kuhuzunisha na kutia huruma kutokana na ajali ya pikipiki aliyoipata
miezi nane iliyopita wakati akienda shuleni.
Norat
alimuambia mwandishi wetu hivi karibuni katika Taasisi ya Mifupa na
Mishipa ya Fahamu (MOI) katika Hospitali ya Muhimbili Jengo la Mwaisela
chumba namba mbili kuwa ajali hiyo aliipata maeneo ya Mtoni kwa Azizi
Ally saa za asubuhi wakati akivuka barabara akienda shule.
Alisema
mara baada ya ajali alipoteza fahamu na alipozinduka alijikuta
amezungukwa na madaktari wa Muhimbili. Katika mahojiano hayo, Norat
alikuwa na haya ya kusema:
“Najua
huu ndiyo mwisho wangu wa kusoma, ndoto ya kufika chuo kikuu imezimika
ghafla kama taa, sikutegemea kama leo hii ningekuwa hivi, nilizaliwa
nikiwa sina matatizo, nilikuwa natembea kwenda shule leo hii siinuki,
nalishwa kama mtoto mdogo,“Mama ndiye ananiogesha, kila kitu juu yake
wakati hana kazi ya kufanya, namuhurumia sana, bora baba angekuwa hai
wangesaidiana kunitunza, pole mama…”Muonekano wa jeraha la mguu baada ya kupata ajali ya pikipiki.
ICU MIEZI MITANO
“Ajali niliyopata ilikuwa mbaya sana, sikutegemea kama leo hii
ningekuwa hai, kinachoniuma ni kuona niko kitandani siinuki wala kukaa,
nimevunjika mguu, kiuno na mbavu napata maumivu kupita kiasi, nipo hapa
wodini lakini ni baada ya kukaa katika chumba maalum cha wagonjwa
mahututi (ICU) ambao wako chini ya uangalizi wa madaktari kwa miezi
mitano.
“Najua
muda si mrefu nitaruhusiwa na madaktari kwenda nyumbani, naamini
nitakufa, sitachukuwa muda mrefu kutokana na umaskini wetu, mahitaji
muhimu sitayapata kwa vile mama hana kazi, tutakula nini, nitavaaje,
nitapataje dawa na tutaishi wapi, nyumba yenyewe ni ya kupanga na kodi
imeisha, tutaelekea wapi sisi jamani!
“Wakati
nikiwa mzima mama alikuwa akizidiwa na majukuma na sasa nimekuwa mlemavu
wa kitandani tena wa kutazamwa muda wote! “Bora ningebakia Muhimbili
kuliko kumhangaisha mama, sijui kodi ya chumba atapata wapi kwani kabla
sijaugua alikuwa akihangaika kufanya biashara ndogondogo na kupata fedha
ya matumizi.”
Norat Rashid akiwa katika jengo la Mwaisela chumba namba mbili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
WALIMU, WANAFUNZI WENZAKE WAMSUSA
“Nikiwa shule wanafunzi wenzangu walikuwa wakinipenda sana, nikiwa
Muhimbili walikuja mara moja tu kuniona nilivyoumia, mpaka leo
sijawaona. Walimu nao walikuja mara moja kwa sasa hawaonekani,
anayenitembelea ni mama peke yake, hata mjomba naye haji sijui kwa nini,
au wananiona kama mzigo kwao?
“Kuna
wagonjwa wanatembelewa na ndugu zao kuwafariji wakati mwingine kuwaletea
chakula lakini kwa upande wangu hakuna wa kunijulia hali, lakini siyo
tatizo kubwa kwangu, yote namwachia Mungu.
“Nawaombeni wananchi mlio na moyo wa huruma mnisaidie, mniombee
niweze kutembea, nirudi shule nisome kama wenzangu,” alisema Norat huku
akitokwa na machozi.
Kwa kuwa Norat hana simu, watakaopenda kumsaidia wakawaone maofisa wa ustawi wa jamii Muhimbili watawaunganisha naye.
Post a Comment