Wakati
wanawake kwa wanaume wengi huenda barani Asia, hasa China kununua bidhaa
kwa ajili ya kuja kuzichuuza, hali sasa ni tofauti kwa kuwa kuna
wasichana ambao huenda huko kwa ahadi za ajira, lakini huishia kufanya
ukahaba kwenye madanguro, gazeti hili linaweza kukuthibitishia.
Wasichana
hao hutafutwa na mawakala wa hapa nchini ambao kazi yao huwa ni
kutafuta wasichana wazuri na baadaye kuwashawishi kwa kuwaeleza fursa za
ajira za hotelini zilizo barani Asia.
Msichana
akikubali, wakala huchukua jukumu la kumtafutia viza ya kuingia China na
baadaye kuwasiliana na mwenyeji wake, maarufu kama Lady Boss, ambaye
hutuma tiketi ya ndege kwa ajili ya kumsafirisha 'mwajiriwa' mpya.
Hata
hivyo, hali hubadilika mara wafikapo huko kwa kuwa 'mwajiri' huyo
humpokonya hati ya kusafiria na baadaye kumpa maelekezo kuwa atatakiwa
kulipa Dola 200 kila siku ambazo atakuwa akizipata kwa kufanya umalaya
kwenye klabu na maeneo ya biashara.
Tayari
wasichana kadhaa wa Kitanzania wamenaswa katika mtego huo na kujikuta
wakilazimika kuuza miili yao ili wamudu ada ya Dola 200 pamoja na fedha
za kujikimu, akiwemo Munira Mathias mwenye umri wa miaka 23 ambaye
alimudu kuvaa ujasiri wa kuweka bayana uovu huo katika mazungumzo yake
na gazeti hili.
Binti
huyo Mtanzania aliyesafiri kwa saa 18 kwenda Guangzou, China alitakiwa
kupumzika kwa saa mbili tu kabla ya kupelekwa kuanza 'kazi' ambayo
hakuitarajia.
"Baada ya kupumzika kwa saa mbili tu, nilipelekwa kwenye klabu," anasema Munira wakati akisimulia mkasa wake.
"Sikuwa
na kazi nyingine zaidi ya kucheza muziki na wanaume ambao licha ya
kwamba sikuwahi kuwaona, walinichangamkia kama vile wananifahamu."
Munira
aliondoka Januari mwaka huu kwenda China ambako aliahidiwa kuwa
angeajiriwa hotelini, lakini alikutana na 'ajira' ya ukahaba, huku
akilazimika kuwalipa 'waajiri' wake Dola za Marekani 200 kila siku.
Binti
huyo, ambaye alifanikiwa kuchomoka mikononi mwa waajiri hao baada ya
viza yake kuisha, alisema kwa siku 91 alizokaa China, alipata mateso
ambayo hatayasahau ikiwamo kupigwa, kubakwa na kundi la wanaume raia wa
Nigeria, pia kulazimika kutoa mimba aliyoipata kwa kubakwa.
"Nilifika
Guangzhou kama saa 9.00 alasiri za China na kulikuwa na baridi sana,"
anasema Munira akisimulia jinsi alivyokanyaga kwa mara ya kwanza ardhi
ya nchi hiyo akiwa na matumaini ya kuanza maisha mapya.
"Wakati huo nilikuwa nikijaribu kupata mawasiliano na mwenyeji wangu ambaye niliagizwa kutoka Magomeni, Dar es Salaam.
Post a Comment