*********
Mvutano mpya umeibuka baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kumvaa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
kikidai ofisi yake inatumiwa na wasaliti wa chama hicho.
Pia, chama hicho kimemtaka Jaji Mutungi ajitokeze
hadharani kubainisha iwapo yeye ndiye aliyemtuma msaidizi wake, Sistyl
Nyahoza kutangaza kuwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk
Willibrod Slaa hawana sifa ya kugombea uongozi ndani ya chama hicho
kutokana na kuzuiwa na katiba ya Chadema.
Jana, Nyahoza alikaririwa na vyombo vya habari
akisema Mbowe na Dk Slaa hawana sifa za kugombea uongozi wa chama hicho
kutokana na katiba ya chama chao kuwabana.
Alibanisha kuwa kipengele cha ukomo wa mgombea
katika katiba yao ya mwaka 2006 kiliondolewa kinyemela bila idhini ya
mkutano mkuu.
Nyahoza alisema katiba ya Chadema ya mwaka 2004,
ilikuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka kuwa kiongozi aliyeongoza
vipindi viwili vya miaka mitano mitano, hawezi kuwania tena nafasi hiyo.
Jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema,
John Mnyika alisema Jaji Mutungi hana mamlaka ya kubaini sifa za
viongozi wa chama hicho, bali wenye mamlaka hayo ni wanachama wa chama
hicho pekee.
Mnyika alisema mwaka 2006, katiba ya Chadema
haikurekebishwa, bali iliundwa upya na kuridhiwa na mkutano mkuu wa
chama na kwamba Agosti 13, 2006 ilizinduliwa na nyaraka zote
alikabidhiwa Msajili wa Vyama wa wakati huo, John Tendwa.
Katika uzinduzi huo wa katiba pamoja na bendera
mpya ya Chadema, Tendwa alikimwagia sifa chama hicho kwa kuonyesha
mwelekeo na mwenendo mzuri na kuvishauri vyama vingine viungane nacho
kuunda chama cha upinzani chenye nguvu nchini.
Akizungumzia mabadiliko hayo, Mbowe alikaririwa na
gazeti hili Agosti 15, 2013 akisema yalikuwa yanalenga kuimarisha
mapambano ya kisiasa ya chama hicho.
Mnyika alisema: “Mkutano mkuu wa chama uliipitisha
Katiba hiyo baada ya mchakato mrefu wa kukusanya maoni kutoka kwa
mabaraza ya wilaya na majimbo. Hatukurekebisha katiba kama inavyoidaiwa.
Ni makubaliano ya wanachama wote ambao waliafikiana na mambo
yaliyotakiwa kuwamo.”
Alisema katika mchakato huo kulikuwa na
makubaliano na mabishano katika baadhi ya masuala lakini suala la ukomo
wa uongozi liliafikiwa na wanachama wote bila tatizo na kupitishwa
kuingia katika katiba na Ofisi ya Msajili ilipelekewa fomu ya
marekebisho pamoja na katiba mpya kama sheria inavyotaka... “Kama
wameipoteza waseme tuwapatie katiba wairejee.”
“Tunachomtaka Mutungi ni kuheshimu katiba ya chama
na kuwaheshimu wanachama wa Chadema na ayapuuze madai ya wasaliti
wachache. Kama vipi asubiri aone uamuzi wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu
ubainishe kama katiba ilivunjwa,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema wameshtushwa na kauli ya ofisi hiyo na kuituhumu kwamba imeanza kutumika kisiasa na wasaliti.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo jana,
Jaji Mtungi alisema: “Hili suala lisimamiwe na chama husika kwa
kuwasiliana na Ofisi ya Msajili… hakuna haja ya kulikuza katika vyombo
vya habari. Wanachama wa Chadema watapata taarifa kutoka kwa viongozi
wao ni nini kinaendelea.”
Kuhusu madai kwamba ofisi yake inatumika kisiasa
alisema: “Kama nilivyosema, hayo tuyaache hii ofisi yetu ipo more
technical (kitaalamu zaidi) hatuingizi siasa. Wao (Chadema) waje kwenye
ofisi yetu tuongee kama taasisi, iwapo tunataka kuwasilisha jambo katika
vyombo vya habari, basi tutaitisha mkutano na waandishi wa habari,”
alisema Mutungi.
Mamlaka ya msajili
Mnyika aligusia pia mamlaka ya msajili huyo
akisema... “Hana mamlaka ya kutangaza sifa za mgombea wa Chadema. Sifa
na uamuzi vimetajwa katika katiba na kanuni za chama. Kifungu cha 6.3.2
cha katiba ya 2006 kinabainisha wazi kuwa kiongozi aliyemaliza muda wake
na mwenye sifa ya kugombea anaruhusiwa kugombea...?” Alisema hata
katika uchaguzi wa ndani wa mwaka 2009 viongozi wengi walichaguliwa na
wakiwa wameshamaliza ukomo wa uongozi na msajili wa vyama hakuzungumza
chochote.
Alisema hawababaishwi wala kuguswa na uamuzi
uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa kwa kuwa mkutano mkuu wa Chadema
unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, ndiyo utakaoamua hatima wa
kiongozi yeyote wa chama hicho.
MWANANCHI
Post a Comment