MAHAKAMA ya Wilaya ya Njombe imetupia mbali kesi iliyokuwa
ikiwakabili viongozi wa CHADEMA mkoani hapa, ya kutishia kummwagia
tindikali Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga (CCM) maarufu kama Jah
People.
Sanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Njombe, alidai kukumbana na tishio hilo wakati wa kampeni za uchaguzi
mdogo wa udiwani Kata ya Njombe mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, mwanasheria wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Malya, alisema kesi hiyo
iliyokuwa chini ya Hakimu Augustino Rwizele, ilitupiliwa mbali kwa
kutumia kifungu cha 91 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Alisema kuwa shitaka la kwanza lililokuwa likiwakabili viongozi hao
ni lile lililotokea Februari 3, mwaka huu, ambapo washitakiwa Ali
Mhagama, Robert Shejamabu na Award Kalonga walidaiwa kuvamia kikao cha
CCM na kutishia kummwagia tindikali mbunge huyo.
Shitaka la pili lilimhusu Emmanuel Mwasongwe ambaye ni msaidizi wa
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, la kutoa lugha ya matusi
dhidi ya Jeshi la Polisi mkoani Njombe.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, viongozi wa CHADEMA waliviomba vyombo
vya dola pamoja na mahakama kuendelea kufanya kazi kwa kufuata maadili
ya kazi zao ili kila mwananchi apate haki yake.
Katibu wa CHADEMA Kata ya Njombe Mjini, Ali Mhagama aliwataka
wananchi kuwa makini katika chaguzi mbalimbali zijazo kwa kuchagua
viongozi ambao watajali maslahi ya umma.
“Tunamshukuru Mungu kwa kushinda kesi hii, na endapo tungepatikana na
hatia leo hii, bila shaka kungekuwa na pengo kubwa katika utendaji wa
kazi za chama,” alisema Mhagama.
Kalonga, alisema pamoja na kupigwa katika tukio hilo kiasi cha
kuvunjwa taya, alishangaa kupelekwa polisi na kufunguliwa mashitaka huku
akiwa ana maumivu makali.
“Siku hiyo nilivunjwa taya, baada ya hapo tulikimbia na kujifungia,
lakini jambo la kushangaza ni kwamba tulipelekwa polisi na
wakatufungulia mashitaka,” alisema Kalonga.
Akizungumza mara baada ya hukumu hiyo, Katibu wa CCM Wilaya ya
Njombe, Clemence Mponzi, alikiri kuwa chama chake kilishindwa kwenda
kutoa ushahidi na hivyo kuifanya mahakama itoe uamuzi wake.
Katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika Februari 9, mwaka huu, CHADEMA
ilishinda kupitia mgombea wake Joseph Mtambo, akichukua nafasi
iliyoachwa wazi na marehemu Lupyana Fute.
Credit: Eddymoblaze blog
Post a Comment