********
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kimesema hakitasubiri wanachama watakaoachwa na
Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uteuzi wa wagombea katika uchaguzi mkuu
ujao.
Kutokana na tamaa ya kuingiza watu wengi kwenye
Bunge, vyama vya upinzani vimekuwa na tabia ya kuwapokea wanachama wa
CCM wanaoshindwa kwenye kura za maoni na baadaye kuwapa nafasi ya
kugombea ubunge, lakini Dk Slaa anasema safari hii hawatakuwa tayari
kufanya hivyo.
“Tulishasema kwamba kwa ngazi zozote hata ngazi
za udiwani au ubunge hatusubiri mabaki, makapi yatakayotokea CCM ndiyo
yaje kwetu,” alisema Dk Slaa katika mahojiano maalumu na Mwananchi
yaliyofanyika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
“Safari hii hatusubiri. Tulishasema kuwa wagombea
wetu tunawaandaa mapema ili tusitegemee mtu anayekuja dakika za mwisho
kuwa ndiyo atuokoe.”
Kauli ya Dk Slaa inaweka msisitizo katika ile
iliyowahi kutolewa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwamba
hawatapokea wanasiasa watakaoihama CCM ili kupata nafasi za uongozi kwa
tiketi ya Chadema.
Katika mahojiano hayo, Dk Slaa alisema: “Huwezi
kuzuia kupokea mwanachama kokote alikotokea, lakini unapofika wakati wa
kuweka watu katika nafasi, lazima ufikirie.”
Mwaka 2010, Chadema ilipokea wagombea wawili
walioshindwa kwenye kura za maoni za CCM, John Shibuda aliyeshindwa
katika kura za maoni za Maswa Magharibi na Freddy Mpendazoe ambaye
alienguliwa kwenye kura za maoni za CCM Jimbo la Segerea.
Shibuda alifanikiwa kurudi bungeni baada ya
kushinda uchaguzi wakati Mpendazoe alishindwa katika hali ya kutatanisha
na juhudi zake za kutengua matokeo hayo mahakamani ziligonga mwamba.
“Tatizo hilo lilitokana na ugeni wetu,” alisema Dk
Slaa akizungumzia kitendo cha Chadema kupokea wagombea walioshindwa CCM
kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
“Lakini kwa wakati huu, Chadema ina wanachama
wengi wenye sifa za kugombea hivyo hatuhitaji kusubiri mtu,” aliongea
katibu huyo mkuu ambaye aliwahi kutangaza kuwa nafasi za wagombea ubunge
wa Chadema katika majimbo yote nchini zitatangazwa kwenye magazeti na
watakaojitokeza, watafanyiwa usaili.
Kuhusu uchaguzi mkuu wa chama hicho, Dk Slaa
alisema utafanyika Desemba mwaka huu baada ya kuridhiwa na kikao cha
Kamati Kuu kitakachofanyika Julai 18.
Alisema wanahakikisha uongozi unapatikana kuanzia
ngazi za chini na watachukua hatua kwa maeneo ambayo watabaini viongozi
wamepeana nyadhifa bila chaguzi madhubuti kufanyika.
Mwananchi
Post a Comment