Wananchi wanaopata huduma za afya katika
kituo cha afya Murongo wilayani Kyerwa mkoani Kagera, wameuomba uongozi
wa kituo hicho kujenga chumba cha kuhifadhia maiti ili kuwaondolea adha
wananchi wanayokumbana nayo baada ya kushuhudia maiti zikilazwa kwenye
vitanda vya wagonjwa.
Wakizungumza na paparazi jana, wananchi
hao walisema kuwa kutokana na kituo hicho kutokuwa na chumba cha
kuhifadhia maiti wameiomba bodi ya afya ili kusaidia ujenzi wa chumba
cha kuhifadhia maiti, kuondoa adha wanayokumbana nayo ya kushuhudia
maiti zikilazwa kwenye vitanda vya wagonjwa.
Mmoja wa wananchi hao, Sebastiani
Katunzi alisema wanapopata msiba katika hospitali hiyo wanakumbana na
changamoto nyingi, kwani maiti zinalazwa kwenye vitanda vya wagonjwa
jambo linalowatia wasiwasi wagonjwa waliopo wodini.
“Tumeiomba bodi ya afya wilayani hapa
isaidie kujenga chumba cha kuhifadhia maiti, kwani watu tunapopata
misiba tunakuwa na wasiwasi, kwani tunashuhudia maiti zikilazwa kwenye
vitanda vya wagonjwa jambo ambalo siyo jema,” alisema Katunzi
Mganga Mkuu wa kituo hicho, Alobogasti
Nkabyemanyira alisema kituo hicho cha afya Morongo tangu kianzishwe
wagonjwa waliokuwa wanalazwa walikuwa ni wachache, hivyo ingetokea
mgonjwa akafariki alikuwa anasafirishwa siku hiyo.
Nkabyemanyira alikiri kuwapo kwa tatizo
hilo la kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti na kueleza kwamba
wagonjwa wameongezeka kiasi kikubwa na kusababisha kuwapo kwa upungufu
wa vitanda pia.
“Ni kweli kuna tatizo, lakini
tutawasilina na uongozi wa wilaya ili bajeti ya mwaka ujao iweze kukidhi
mahitaji kama hayo,” alisema Dk Nkabyemanyira.
Loading...
Post a Comment