TUHUMA za ubabe
na usultani wa baadhi ya viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), bado umeendelea kukitesa na kukipasua vipande chama hicho.
Hatua hiyo
imetokana na baadhi ya viongozi, akiwemo Mwenyekiti wake Taifa, Freeman
Mbowe, kupigwa ‘stop’ kuwania tena nafasi hiyo baada ya kubainika Katiba
ya CHADEMA imechakachuliwa ili kuondoa kipengele cha ukomo wa viongozi.
Tayari Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imesema Katibu Mkuu Dk. Willibroad
Slaa na Mbowe hawana sifa za kugombea tena uongozi wa chama hicho kwa
kuwa Katiba haiwaruhusu.
Hatua hiyo
imetokana na malalamiko yaliyowasilishwa na baadhi ya wanachama wa
CHADEMA, akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wake mkoa wa Arusha, Samson
Mwigamba.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mwigamba alisema ukweli kuhusu ubabe na usultani ndani ya CHADEMA umedhihirika.
“Nashukuru
Mungu ukweli wa mambo ndani ya CHADEMA sasa umedhihirika. Nilitukanwa na
kupewa majina yote mabaya, lakini demokrasia na uhuru niliokuwa
naupigania umeonekana,” alisema Mwigamba.
Alisema
alibaini kuwa viongozi wamechakachua Katiba ya CHADEMA baada ya Mbowe
kujitokeza hadharani na kuanza kupambana na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuongoza chama hicho,
katika nafasi ya uenyekiti.
Alisema kwa
mujibu wa katiba, Mbowe hakuwa na sifa za kuendelea kugombea kwa kuwa
alishafikia ukomo wa uongozi, hivyo alipofuatilia alibaini vipengele
vimebadilishwa kinyemela bila kushirikisha vikao halali.
Alisema baada
ya kubaini hilo, viongozi wa juu walianza kumdhibiti ikiwa ni pamoja na
kumvua nyadhifa zake ili asiingie kwenye vikao vya maamuzi.
“Nilianza
kuwekewa mizengwe ya kila aina, nikatafuta muhtasari wa vikao kadhaa,
lakini sikuona vipengele vilivyobadilishwa kuhusu uongozi. Ila Katiba
iliguswa kipengele hicho hivyo, kwa kushirikiana na wenzangu, tukapeleka
malalamiko kwa msajili kwa hatua zaidi,” aliongeza Mwigamba ambaye kwa
sasa ni mwanachama wa ACT Tanzania.
Mwigamba
alisema baadhi ya wanachama hususan vijana hawakumwelewa wakati
akipigania haki hiyo na wengine walitumia mitandao ya kijamii na vyombo
vya habari kumdhihaki.
“Nikiwa kituo
changu cha Arusha, nilikuwa naona mambo kawaida, lakini nilihamia makao
makuu ndipo nikaona hiki chama kinaendeshwa kiajabu. Hakiwezi kushika
dola wakati kimejaa uozo na kukiuka misingi na taratibu zake,” alisema
na kuongeza: “Viongozi ni wabinafsi, wanajijali wenyewe hivyo nikaanza
kupigania mabadiliko ili tuweze kusonga mbele”.
Alisema mwisho
wa CHADEMA utafika baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Mdhibiti Mkuu na
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu mapato na matumizi ya chama
hicho.
Alisema kuna
ufisadi mkubwa ndani ya CHADEMA, ambapo fedha za umma zinazotolewa kama
ruzuku, zimekuwa zikitafunwa na wachache na hakuna hesabu zinazoeleweka.
Wiki iliyopita
baadhi ya wanachama wa CHADEMA, wakiwemo wajumbe wa Baraza Kuu na
Mkutano Mkuu, waliandamana na kuwasilisha malalamiko dhidi ya viongozi
wao kwa msajili na CAG.
Huku wakiwa na
mabango, wajumbe hao walitaka ofisi hiyo kuubana uongozi wa CHADEMA
kuhusu kukiuka Katiba na matumizi mabaya ya fedha za ruzuku na madaraka.
Hata hivyo, kwa
nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John
Mnyika, amekuwa akiwaponda kuwa ni mamluki na kuwa wametumwa na CCM.
Naye Mbunge wa
Wawi, Hamad Rashid Mohamed, alisema vyama vya upinzani nchini
vinajitahidi kuikosoa serikali, lakini vyenyewe vimeoza.
Alitolea mfano
baadhi ya wabunge wa CHADEMA waliodai kuwa Katiba ya Tanzania imekaa
kisultani, huku wakificha usultani ulioota mizizi ndani ya vyama vyao.
“Hata hao wanaosema wanaweka mazingira ya wengine kugombea uongozi, bado vikwazo ni vingi, hata wanachama
kuogopa kujitokeza na watu wanapita bila kupingwa. Kabla ya kulaumu ni
vyema tukajiangalia wenyewe kwani, nyumba zetu ni chafu,” alisema.
Wasomi waponda
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, amesema vyama vya upinzani
vinaweza kusambaratika kutokana na usultani uliokithiri.
Alisema vyama
hivyo vinapaswa kuiga sera na mipango kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM),
ambazo ndizo zinakifanya kuendelea kutawala kwa miaka mingi.
Alisema vyama
vingi vya siasa vilianzishwa na watu ambao wamekuwa wakitumia umaarufu
wao kung’ang’ania madaraka na kwamba, ndio sababu ya migogoro ya mara
kwa mara.
Kuhusu uamuzi
wa Ofisa ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Bakari alisema ni mwafaka na
anauafiki kwa kuwa vyama hivyo vilianzishwa kwa sheria namba nne ya
mwaka 1992 na lazima ifuatwe.
Naye Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Alli, alisema uamuzi wa msajili
ni mtihani kwa CHADEMA na wanapaswa kuangalia namna ya kuumaliza.
Alisema vyama vingi vya siasa vinakosa sura ya utaifa na migogoro inayotawala ndani ya vyama hivyo inaweza kuvisambaratisha.
Alisema vyama vingine ukiacha CCM, vimekuwa havifanyi vizuri katika kubadilisha nafasi ya mwenyekiti.
Bashiru alisema mgogoro wa CHADEMA ulianza tangu enzi za marehemu Chacha Wangwe na umeendelea na kuhamia kwa Kabwe.
“Vyama hivi
havifanyi vizuri katika kubadilisha mwenyekiti na vimekuwa vikikabiliwa
na migogoro hata wakati wa kuteua wagombea katika uchaguzi. Kwa kiasi
kikubwa vingi vinakabiliwa na ukiritimba wa demokrasia,” alisema.
Katibu wa Jimbo, vigogo wa kata tisa waachia ngazi
Katika hatua
nyingine, CHADEMA imeendelea kusambaratika baada ya Katibu wa Jimbo la
Mpanda Mjini, Joseph Mona na viongozi wa kata tisa za wilaya ya Mpanda,
kuachia ngazi.
Viongozi hao walibwaga manyanga juzi na kuweka hadharani kuwa, majungu na udikteta wa viongozi wa juu umewashinda.
Wakizungumza
baada ya kutangaza kuachia ngazi na kujivua uanachama, viongozi hao
walisema uendeshaji holela wa chama hicho, ikiwemo matumizi mabaya ya
fedha ni miongoni mwa mambo yaliyowakimbiza.
Mona aliliambia
gazeti hili jana kuwa, alishindwa kuendelea kuliongoza jimbo hilo kwa
sababu viongozi wake ni wababe na hawashauriki.
Alitaja majina
ya kata ambazo wenyeviti na makatibu wake walijiuzulu juzi kuwa ni
Ilembo, Kasamlili, Makanyagio, Misunkumilo, Shamwe, Kakese, Kawajense na
Mpanda Hoteli.
“Tunapiga
kelele za kutaka mabadiliko kwenye serikali, lakini ndani ya taasisi
yetu kumeoza na hakutamaniki. Chama kinaendeshwa kwa hisia, ikionekana
mwanachama anataka mabadiliko anafukuzwa,” alisema Mona na kuongeza:
“Jimbo letu lina mbunge, lakini katika kipindi cha miaka tisa tumepewa
ruzuku ya sh. milioni 16 tu ila kila mwezi tunaletewa fomu za marejesho,
sasa hizo fedha zinakwenda wapi.”
Naye Wastara
Feruzi, ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jimbo la Mpanda
Mjini, alisema sababu za kujiuzulu ni kuchoshwa na majungu.
Chanzo: Gazeti la Uhuru
Chanzo: Gazeti la Uhuru
Post a Comment