Katibu
wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa
habari leo (hawapo pichani ) kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalum la
Katiba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika
ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za Bunge jijini Dares Salaam.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu wa Bunge Maalum la Katiba,
Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani )
kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba kwa niaba ya Mwenyekiti
wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo
za Bunge jijini Dares Salaam.
Picha na Magreth Kinabo – MAELEZO
…………………………………………………………………………………
Na Winner Abraham na Rose Masaka-MAELEZO-Dar es salaam
Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa Mkutano wa Bunge
hilo, utaendelea kama ulivyopangwa Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.
Amesema
kuwa licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea na msimamo wao
wa kutaka kususia vikao vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado
kuna mambo muhimu ya kujadiliwa.
Mwenyekiti
huyo ametoa kauli hiyo leo mjini Dar es salaam, katika taarifa yake
iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya
Khamis wakati wa mkutano wa waandishi wa habari.
“Kamati
hiyo, imeamua kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi kwamba Bunge Maalum
la Katiba liendelee kwa sababu yapo masuala mengi muhimu ya kikatiba
ambayo yanatuunganisha kama vile usawa wa kijinsia katika nafasi za
uongozi na kuikarabati Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC).
“Mambo
mengine ni kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano,haki za
wakulima,wafugaji,wasanii na makundi mengineyo na ukomo wa vipindi vya
uongozi,”alisema Sitta katika taarifa hiyo.
Aidha
aliongeza kwamba uamuazi huo, umefikiwa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo
waliohuduria ambao walikuwa zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe
wote, ambapo waliendelea na kikao.
Alisema
hatua ya baadhi ya wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa
siyo muafaka na si wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku
za usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri
unavyojitokeza.
Aliongeza
kwamba Kamati hiyo, inaona kwamba kwa kuendelea kulisusia Bunge hilo,
na kupuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu
ya dini inatilia shaka dhamira halisi ya viongozi wa kundi hili la
wasusiaji kupuuzia juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu
lengo la ususiaji kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni nyingine na
siyo upatikanaji wa Katiba.
Alisema
Kamati hiyo inarejea kwamba wajumbe hao 629 wamekabidhiwa jukumu
adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania jukumu ambalo hutokea
baada ya miongo kadhaa ya uhai wa Taifa lolote.
“ Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisisitiza.
Mwenyekiti
huyo alisema katika ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa
Bunge hilo, uzingatie upya baadhi ya Kanuni za Bunge hilo, ambazo ni
kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na hatimaye
inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati
ya hizo siku 60 ni za nyongeza na tatu zilizokuwa pungufu za siku 70 za
awali.
Alisema
Kamati hiyo, inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia mikutano ya
Bunge hilo, kurejea katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo lina uwezo wa
kisheria wa kutatua matatizo yaliyopo.
Amesema kuwa
kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na tano ya Kanuni za Bunge
Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya wajumbe thelathini
(30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika mkutano ulipita
lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi,walikisusa
kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.
“Jitihada
mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na mwenyekiti hadi
asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza kuwashawishi wajumbe hao wasusiaji
kuhudhuria kikao, alisema Sitta katika taarifa yake.
Aliitaja
athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa kuandaa na hatimaye
kuipigia kura Katiba mpya ni pamoja na kupoteza mabilioni ya fedha
za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi, baya zaidi ni kuiweka
rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno mgogoro wa katiba na kuwagawa
wananchi kwa propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015
Post a Comment