JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA USHIRIKIANO WA
AFRIKA MASHARIKI
Tanzania imeridhia rasmi Itifaki ya Umoja wa
Fedha ambayo ni sheria muhimu katika utekelezaji wa hatua ya tatu ya Mtangamano
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Itifaki hiyo iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 25 Juni
2014.
Itifaki ya Umoja wa Fedha ilisainiwa na Wakuu
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Novemba 30, 2013 Jijini Kampala, Uganda
wakati wa Mkutano wa 15 wa Kilele wa Wakuu wa Nchi hizo. Baada ya kusainiwa na
Wakuu wa Nchi, Nchi wanachama zilitakiwa ziwe zimeridhia Itifaki hiyo ifikapo Julai
1, 2014 ili kuruhusu kuanza kwa utekelezaji wake.
Baada ya kuridhiwa kwa Itifaki, Nchi wanachama
zitatakiwa kufuata mpango mkakati wa utekelezaji ambao umeelezwa bayana kwenye
Itifaki hiyo.
Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha
utapelekea Nchi wanachama yaani Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda kuwa
na sarafu moja ifikapo mwaka 2024. Ili kufikia hatua ya kuwa na sarafu moja
mwaka 2024 baadhi ya mambo muhimu yanayotakiwa kufanyika ni pamoja na
uanzishwaji wa Taasisi za Kifedha.
Taasisi hizo ni pamoja na Taasisi ya Fedha ya
Afrika Mashariki (ambayo baadaye itakua Benki Kuu ya Afrika Mashariki), Taasi
ya Takwimu ya Afrika Mashariki, Tume ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Udhibiti na
Tume ya Huduma za Kifedha ya Afrika Mashariki.
Utekelezaji wa Itifaki utahusisha pia
uhuishaji wa sera zao za kifedha zikiwemo za kubadilisha fedha, sera za malipo
kupitia benki, sera zinazohusu uzalishaji na usambazaji wa takwimu na sera za
masoko ya fedha.
Izingatiwe kuwa, kabla ya kuingia kwenye Sarafu
moja mwaka 2024, nchi wanachama zitatakiwa kukidhi vigezo vya Muunganiko wa
uchumi mpana (Microeconomic Convergence Criteria) vilivyowekwa ambavyo ni pamoja na:
i. kuwa na mfumuko wa bei
usiozidi 8%;
ii. Kuwa na nakisi ya Bajeti
isiyozidi 3% (pamoja na misaada);
iii.
Kuwa na deni la taifa
lisilozidi 50% ya Pato la Taifa;
iv. Kuwa na akiba ya fedha
za kigeni ambazo zinatosheleza manunuzi ya bidhaa kutoka nje kwa kipindi cha
miezi minne na nusu.
Vigezo hivyo vinatakiwa kutekelezwa kwa kipindi
cha miaka mitatu mfululizo kukaribia 2024. Kama kutakua angalau na nchi tatu za
Jumuiya zitakazoweza kufikia vigezo hivyo basi zitaweza kuanza kutumia sarafu
moja.
Umoja wa Fedha ni hatua ya tatu ya Mtangamano wa
Afrika Mashariki baada ya hatua za awali, Umoja wa Forodha (2005) na Soko la
Pamoja (2010) kutekelezwa. Hata hivyo ili hatua ya Umoja wa Fedha iweze
kufanikiwa inategemea utekelezaji wa hatua za awali za mtangamano na ushiriki
wa wananchi katika kuzitumia fursa zitokanazo na mtangamano. Wizara
inawahamasisha Watanzania kutumia fursa mbalimbali zitokanazo na Umoja wa
Forodha na Soko la Pamoja.
Imetolewa na
KATIBU MKUU
WIZARA YA USHIRIKIANO WA
AFRIKA MASHARIKI
Post a Comment