IMG_2163

Katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mbeya, Bashiru  Madodi.

Na Mwandishi wetu

Katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), mkoa wa Mbeya, Bashiru  Madodi, amesema kuwa tatizo kubwa la baadhi ya vijana wa chama hicho(UVCCM), wanatumika vibaya na wagombea na kukisemea chama bila utaratibu.Madodi alisema hayo katika ukumbi wa CCM mkoa wa Mbeya, wakati wa Baraza kuu la UVCCM Mkoani hapa, ambalo lilifanyika kwa mujibu wa kanuni za umoja huo kwa ajili ya maandalizi ya kumwapisha kamanda wa Vijana hao mkoa wa Mbeya, Yona Sonelo na makamanda wa wilaya zote tisa za mkoa huo.Kauli ya Madodi imetafsiriwa kama anamjibu Katibu wa hamasa wa UVCCM Taifa, Paul Makonda, ambaye hivi karibuni ametoa tamko kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzuru, Edward Lowassa kuwa hafai kuwania nafasi ya Rais wa Tanzania, alisema kuwa inashangaza vijana kuenda mbio na kutoa matamko ambayo yanapaswa yatolewe na vikao vya chama kwanza.



Alisema kuwa, vijana wengi wanatembea na wanaotaka madaraka, kutokana na vijana kuwa ndiyo tegemea la taifa, kwasababu wanaweza kukimbia huku na kule.

“Ni kipindi kigumu sana kwenu, wakati wetu akina Guninita waliwahi kufutwa uongozi kutokana na tabia zinazofanana na vijana wa leo. Mnatoa matamko bila hata vikao vya chama kutoa maamuzi” alisema huku akishangiliwa.

 “Makonda anatakiwa atafsiri vema kauli ya Madodi na kurejea kwenye misingi ya kanuni ili aweze kufanya vema kazi za jumuiya yake ya watoto badala ya kila wakati kuinuka na kutoa matamko ambayo yanaashiria yupo na kiongozi mmoja mfukoni kutafuta nafasi ya Rais mwaka 2015”

Kwa upande wake, Paul Makonda ambaye alikuwepo kwenye Baraza hilo, ndiye aliyeanza kueleza kuwa vijana wapo ndani ya mifuko ya wanasiasa wakubwa, ndiyo maana inafiia mahala chama hakiwaamini. 

Alisisitiza kuwa, kuna baadhi wanaomtuhumu kuwa yeye anatumwa na kundi la watu kutoa matamko, jambo ambalo siyo la kweli bali anaongozwa na akili zake mwenyewe na madhara ya magenge ni kujitafutia riziki binafsi.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, alisema kuwa vijana wangoje chama kitoe maamuzi kwanza ya mgombea nafasi ya Urais ndipo vijana wamuunge mkono mtu huyo, badala ya kugawanyika kwa sasa.

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo chakula na ushirika, Godfrey Zambi, alisisitiza umoja miongozi mwa Jumuiya hiyo ya vijana kwa maslahi ya chama na Taifa.