*Wazazi watathmini ujuzi wa watoto japo ni wa chini ila kwa usahihi.
*Na wala hawaoneshi kudai kubadili hali hii katika siku zijazo
*Na wala hawaoneshi kudai kubadili hali hii katika siku zijazo
Mwananchi
1 tu kati ya 10 ndiye anayefikiri kuwa watoto wengi wanaomaliza darasa
la 2 wana uwezo wa kusoma na kufanya hisabati wa darasa hilo hilo (ngazi
ya darasa la 2). Mbaya zaidi, wananchi 3 tu kati ya 10 (31%) wanafikiri
kuwa watoto hawa wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuhesabu kwenye
ngazi yao; ikimaanisha kuwa wananchi hawana matumaini kama kweli mfumo
wa elimu utawafundisha watoto ujuzi na stadi wanazotakiwa kupata wakiwa
shuleni.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Nini kinaendelea kwenye shule zetu? Wananchi watafakari juu ya hali ya elimu.
Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa
kwanza Afrika kwa njia ya simu mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa
ambao unauwakilishi wa kaya zote Tanzania Bara.
Muhtasari huu unachunguza hali
ya shule zetu, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ushiriki wa wazazi
kwenye elimu ya watoto wao. Licha ya matarajio ya chini kwenye mfumo wa
elimu, wazazi mara nyingi hutimiza wajibu wao kuhamasisha na kusimamia
ujifunzaji. Wanafunzi 7 kati ya 10 waliripoti kuwa wazazi wao hupitia na
kukagua madaftari yao mara kwa mara.
Walimu wana wajibu wa
kuhakikisha watoto wanajifunza shuleni. Hata hivyo, hawawezi kufanya
kazi hii kama walimu wenyewe hawaingii darasani. Wanafunzi 3 kati ya 10
walithibitisha kuwa mwalimu wao muhimu aliingia darasani vipindi vyote
siku iliyopita. Wanafunzi 4 kati ya 10 (38%) waliripoti kuwa mwalimu wao
hakuingia darasani siku nzima, na wanafunzi 3 kati ya 10 (28%) walisema
kuwa, mwalimu aliingia baadhi ya vipindi tu vya siku hiyo.
Sauti za Wananchi iliuliza pia
maswali kuhusu hali ya mazingira ya shule. Karibu wanafunzi wote (99%)
wanafundishwa wakiwa madarasani, siyo nje, na wanafunzi 9 kati ya 10
(91%) hukaa kwenye fomu au dawati shuleni. Hata hivyo, ni nusu tu ya
idadi ya wanafunzi (49%) waliosema hupewa chakula shuleni. Ingawa
kukosekana kwa viti na madarasa kuna uwezekano wa kuathiri viwango vya
kujifunza, watoto wanapokuwa na njaa wanakuwa na uwezo mdogo kupokea na
kumiliki maarifa mapya.
Njia nyingine ambayo watoto
huhifadhi maarifa ni kupitia kazi za masomo kufanyia nyumbani. Kazi hizi
za masomo nyumbani husaidia wanafunzi kukumbuka na kupitia upya masomo
ya siku hiyo na kufanya mazoezi elimishi ya yale waliyojifunza akiwa
mwenyewe. Hata hivyo, wanafunzi 7 kati ya 10 (69%) waliripoti kuwa ni
mara chache sana (au hawapewi kabisa) kazi za masomo za kufanyia
nyumbani. Wakipewa kazi za masomo nyumbani, wanafunzi walisema kuwa mara
nyingi kazi hizo husahihishwa.
Hivi karibuni Tanzania
ilizindua Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mpango huo umeiweka
sekta ya elimu kuwa moja ya vipaumbele vyake muhimu. Sauti za Wananchi
iligundua kuwa ni mtu 1 tu kati ya 7 (16%) ndiye aliyewahi kusikia
kuhusu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema "Utafiti
wa Serikali na utafiti wetu (Uwezo) umeonesha kuwa watoto wako shuleni
lakini hawajifunzi. Utafiti huu pia umegundua hali ya kutisha- theluthi
mbili ya walimu hawaingii madarasani kwa siku nzima au baadhi ya
vipindi. Hali mbaya ya mfumo wetu wa elimu sasa ni jambo la kawaida
kiasi kwamba wazazi hawatarajii kama watoto watajifunza stadi wanaopaswa
kujua. Kama tutaendelea katika hali hii, tutakuwa na kesho isiyo na
mafanikio. Ingawa mpango kama BRN unatafuta kuinua ubora wa elimu, haiko
wazi masuala gani ni kipaumbele muhimu kwa hali ya sasa."
"Kila
shilingi inayotumika kwenye elimu inaweza kutumika mara moja tu. Kama
raia wa nchi hii tunapaswa kudai kuwa sera zote za elimu, jitihada,
vitendo na hatua kwa uaminifu kabisa zijikite kuboresha matokeo ya
kujifunza. Bila kufanya hivyo, hakuna uhakika kwamba thamani ya fedha
itapatikana. Kwa maneno mengine, watunga sera wanapaswa kutumia ushahidi
kuwashawishi walipa kodi, Washirika wa sekta na wanasiasa kuwa fedha za
kodi zinatumika kwenye sera zinazoleta manufaa na ambazo "zinanunua"
matokeo ya kujifunza.”
Imechotwa: Mafoto web
Post a Comment