Ifikapo
Tusije tukajidanganya kama tusipofanikiwa tutaendelea kwa usalama, kuna
hatari ya amani ya nchi na usalama kuvurugika” Warioba
*****
Dar es Salaam. Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
amewataka viongozi wa vyama vya siasa kukutana na kufikia makubaliano
ili mchakato wa Katiba uendelee hatimaye kupatikana kwa Katiba Mpya kwa
masilahi ya Taifa.
Pia, Jaji
Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu amemshauri Rais Jakaya Kikwete na
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuchukua hatua zitakazoondoa
matatizo katika Bunge Maalumu la Katiba ili kuwezesha mchakato huo
kukamilika.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Warioba
alisema ni muhimu viongozi hao kuweka kando tofauti zao za mawazo na
mitizamo ili kupata Katiba Mpya kwa masilahi ya taifa.
Warioba
ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, ameonya kwamba ikiwa
viongozi hao hawataweka kando tofauti zao na kuwezesha Taifa kupata
Katiba Mpya, amani ya Taifa inaweza kuvurugika.
“Tunatoa
wito kwa viongozi wa vyama wakutane watafakari hali ilivyo na kufikia
makubaliano ili mchakato uendelee. Tunafikiri ni jambo bora wakarudi na
usiwepo mjadala wa kuangalia idadi ya kura katika kufikia uamuzi, lengo
lisiwe idadi ya kura, bali makubaliano ya kupata Katiba Mpya,” alisema
jaji Warioba na kubainisha:
“Kipindi
chote, sisi tuliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tulikuwa
tukifuatilia kwa karibu sana mchakato unavyoendelea. Sisi ni wadau
wakubwa, tulitumia miaka miwili kwa maandalizi, tuna hamu kubwa na
matumaini ya kuona sasa Katiba Mpya inapatikana.”
Rais Kikwete na Dk Shein
Jaji
Warioba alisema Rais Kikwete ndiye aliyeanzisha mchakato wa Katiba Mpya
kwa nia njema na kwamba muda wote amekuwa akifanya kazi ya kuusimamia
mchakato huo pamoja na kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba
akishirikiana kwa karibu na Dk Shein, hivyo bado wana wajibu wa kuchukua
hatua ili kukamilisha safari ya kupata Katiba.
“Sasa
Bunge la Katiba lina matatizo, bado ni wajibu wao (Rais Kikwete na Dk
Shein), kuchukua hatua ili kupata Katiba Mpya. Huu ni mchakato, awamu ya
kwanza Bunge lilitunga sheria, ya pili Tume ya Katiba ikafanya kazi, ya
tatu Bunge Maalumu la Katiba na nne wananchi watapiga kura. Mawazo yetu
ni kusaidia mchakato huu ukamilike. Tunataka ufanikiwe,” alisema
akionya:
“Tusije
tukajidanganya kama tusipofanikiwa tutaendelea kwa usalama, kuna hatari
ya amani ya nchi na usalama kuvurugika. Viongozi lazima waelewe hili
kwani madai ya Katiba Mpya yalikuwapo zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Wananchi wengi wanaamini kuna umuhimu wa kupata Katiba Mpya, tena wengi
wa hali ya chini, ingawa viongozi ndiyo walioanzisha madai hayo.”
Kauli
hiyo ya Warioba imekuja huku maandalizi ya kikao cha Bunge la Katiba
linalotarajiwa kuanza tena vikao vyake Agosti tano yakiendelea.
Aprili
16, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliiongoza Ukawa kutoka
kwenye Bunge la Katiba akilalamikia CCM kutowatendea haki kwa mambo
mbalimbali ikiwamo kupinga mapendekezo yao hata ya msingi, akisema
hawawezi kuwa sehemu ya watu wanaosambaza chuki na kuwa sehemu ya
kuibomoa nchi.
Siku
chache baadaye, walianza kufanya mikutano nchi nzima kwa kile walichodai
kuwaeleza wananchi namna CCM inavyotaka kuchakachua maoni yao
yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa
upande wake, CCM imekuwa ikifanya mikutano kuzunguka nchi nzima kueleza
msimamo wake na sababu za wao kutaka kuendelea kutumika kwa muundo wa
Serikali mbili unaotumika sasa na kubeza hoja za Ukawa.
Lakini
jana Warioba alisema yeye na waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
walifuatilia hali ilivyokuwa katika Bunge Maalumu la Katiba na baada ya
kuahirishwa... “Tukaamua tukutane kwa siku tatu kama raia na kufanya
tathmini kama raia, pia tuliamua kukaribisha wasomi na baadhi ya wabunge
wa Bunge la Katiba. Tuliwaalika wasomi watano na wabunge wawili wa
Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale Mwiru na Profesa Abdul Sharif
wa Zanzibar.
“Baada ya
kuwasikiliza, tukafanya tafsiri yetu wenyewe na kufikia mahali tukasema
ni muhimu jukumu la Bunge Maalumu la Katiba kuendelea. Liendelee kwa
msingi wa kuimarisha mchakato wa Katiba Mpya, walifahamu hili, wafikie
makubaliano.
“Waangalie
wapi wanatofautiana, wapi wanakwenda sawa, waweke kando tofauti watoke
na yanayowapatanisha ili kupata matokeo ya kuwa na Katiba Mpya.”
Serikali mbili au tatu
Jaji
Warioba alisema kipindi kilichopita Bunge hilo lilishughulikia kanuni na
kujikita zaidi katika mjadala wa muundo wa Serikali mbili au tatu,
mambo yaliyochukua muda zaidi, lakini mkutano ujao utakuwa na mambo
mengi zaidi.
“Muundo
wa serikali mbili au tatu huo ulikuwa ndiyo mjadala. Katika eneo hilo
hata bunge lijalo kazi bado kubwa inahitajika. Tunaweza kuzungumzia
upungufu wa Serikali tatu, lakini bado kuna umuhimu wa kuzungumzia
udhaifu wa Serikali mbili:
“Bado
matatizo ya Tanganyika kuvaa koti la muungano, mgongano wa Katiba ya
Zanzibar na Muungano, hatuwezi kunyamaza tukaamini yataondoka. Pia lipo
suala la maadili na miiko ya viongozi,” alisema.
Warioba
aliyefanya kazi katika Serikali tangu Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius
Nyerere, alitaja mambo mengine muhimu kuangaliwa katika Bunge hilo kuwa
ni utengano wa mihimili akisema lina mtizamo tofauti, madaraka ya rais,
ukomo wa uongozi na madaraka ya wananchi kuweka au kuondoa mbunge
madarakani, Tume huru ya uchaguzi, Tume ya Haki za Binadamu na suala la
mgombea binafsi.
Mwananchi
Post a Comment