Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
WAZIRI MKUU: OMBEENI TAIFA NA UCHAGUZI MKUU
UJAO
*Askofu
Niwemugizi ataka UKAWA warudi bungeni mwezi ujao, asema siyo ombi.
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini kote nchini na wananchi waungane
pamoja ili kuombea uchaguzi mkuu wa viongozi wakuu wa Rais, wabunge na madiwani
unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumanne, Julai mosi, 2014) wakati
akizungumza na maelfu ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya
Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu
Tarsicius Ngalalekumtwa katika uwanja wa Kichangani wa Kanisa Kuu la Kihesa.
"Maaskofu wote mliopo hapa, najua mnavyoipenda Tanzania...
kila kanisa lina sala maalum ya kuliombea Taifa na viongozi wake, ninawaomba
viongozi wetu mliombee Taifa letu ili mambo yaende salama na hasa uchaguzi wa
mwakani," alisema.
Akirejea mahubiri yaliyotolewa kwenye ibada hiyo na Mhashamu
Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo Katoliki la Tabora ambaye alitoa mfano wa
Daudi na Goliathi, Waziri Mkuu alimfananisha Goliathi na masuala ya rushwa,
ubinafsi na tabia ya viongozi kutojali wananchi wa hali ya chini.
"Viongozi tusipokuwa waadilifu, tukawa wala rushwa na
hatujali wananchi wa hali ya chini tutakuwa sawa na Goliathi. Nawasihi sana
ombeeni Taifa hili na uchaguzi mkuu ujao ili Mungu atupe Daudi atakayeweza
kuliongoza Taifa hili na kulipeleka kunakostahili," alisema huku
akishangiliwa.
Waziri
Mkuu ambaye alihudhuria sherehe hizo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, ametumia
fursa hiyo pia kuwaomba wote kwa pamoja waendelee kuliombea Taifa katika
kipindi hiki cha mchakato wa kuandaa Katiba Mpya. "Watanzania wote tuwe na
moyo wa kuvumiliana na kupendana. Tumuombe Mungu atuwezeshe kupata Katiba mpya
katika hali ya maelewano na amani. Tuombee Taifa na tuombee Watanzania ili
tusije tukatoka katika mstari."
Alisema
ushauri uliotolewa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severini Niwemugizi wa
kuwataaka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba warejee mara moja ni wa muhimu.
"Ushauri wa Baba Askofu ni wa makini, turudi tukabishane pale ndani,
lakini pamoja na yote sheria inasema mwamuzi wa mwisho ni Watanzania kupitia
kura ya maoni. Wale tuliopewa dhamana ya kupitia rasimu turudi pale
tuikamilishe ili Watanzania waweze kupata fursa ya kupiga kura ya maoni,"
alisema.
Mapema, akiwasilisha salamu kutoka Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini Niwemugizi wa Jimbo la
Ngara aliwataka wajumbe wa Bunge maalum la Katiba kurejea kwenye mkutano wake
uliopangwa kuanza Agosti 5, mwaka huu.
"Ninatumia
neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee bungeni mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au
kufanya mizengwe mingine na kutupatia Katiba isiyotufaa, nitawaomba Watanzania
wote tuweke uzalendo mbele na kuikataa rasimu ya Katiba itakayoletwa na pia
tuwanyime uongozi katika uchaguzi mkuu ujao," alisema.
Aliwataka
Watanzania wajitokeze kwa wingi wakati wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga
kura. "Watanzania tuna tabia ya kudharau siasa. Tusidharau masuala ya
siasa kwa sababu ni muhimu na yanagusa maisha yako na yangu, yanagusa maisha ya
watoto wako," alisema.
Sherehe
hizo za jubilei ya miaka 25, zilihudhuriwa na maaskofu 19 kutoka majimbo
mbalimbali ya kanisa katoliki hapa nchini, wawakilishi wa maaskofu watatu na
abate mmoja. Viongozi wa kitaifa waliohudhuria ni Spika wa Bunge, Mama Anne
Makinda; Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa; Waziri Mkuu
mstaafu, Edward Lowassa na baadhi ya wabunge wa mkoa wa Iringa.
Askofu
Ngalalekumtwa (66) alipata upadrisho Aprili 7, 1973 huko San Ginesio, Camerino,
nchini Italia na kupata daraja ya uaskofu mwaka 1988 ambapo alisimikwa rasmi
Januari 1989 kuwa Askofu wa Jimbo la Sumbawanga.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE,
JULAI MOSI, 2014
Post a Comment