********
Moshi. Askofu wa Kanisa la Christian Fellowship Assemblies of
God la Arusha, Jumanne Kilongola amehukumiwa kifungo cha miaka 32 jela
baada ya kupatikana na hatia ya kupora Sh5.3 bilioni ndani ya Benki ya
NBC, Tawi la Moshi Mei 21, 2004.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa jana na Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimanjaro, Simon Kobelo,
askofu huyo amehukumiwa kifungo hicho pamoja na raia watano wa Kenya
baada ya kupatikana na hatia ya kufanya wizi huo kwa mtutu wa bunduki.
Kati ya fedha hizo, Sh126.2 milioni zilikuwa mali
ya Benki ya NBC wakati Sh5.1 bilioni ni mali ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) ambayo ilikuwa ikitumia NBC Moshi kama kituo chake kidogo.
Ilielezwa mahakamani hapo wakati wa ushahidi kuwa
Askofu Kilongola ndiye aliyekodi gari aina ya Toyota Landcruiser
lililotumiwa kubeba fedha hizo kwa Sh320,000 na alimweleza mmiliki wake
kuwa alikuwa anakwenda kubeba wanakwaya wake.
Raia wa Kenya waliohukumiwa kifungo hicho cha
miaka 32 ni Wilfred Onyango Nganyi, Patrick Muthee Murithi, Gabriel
Kungu Kariuki, Jimmy Maina Njoroge na Simon Ndungu Kiambuthi.
Hata hivyo, mahakama hiyo iliwaachia huru raia
wengine watatu wa Kenya, Boniface Mwangi Mburu, David Ngugi Mburu na
Michael Mbanya Wathigo kutokana na kukosekana ushahidi dhidi yao.
Hakimu Kobelo alisema upande wa mashtaka
ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Hyra Sande, Ladslaus Komanya na
Stella Majaliwa umethibitisha pasipo shaka kuwa washtakiwa hao
waliohukumiwa walitenda makosa hayo.
Alisema ushahidi dhidi ya Askofu Kilongola na raia
hao wa Kenya ulikuwa madhubuti kutokana na kutambuliwa kikamilifu na
mashahidi katika gwaride la utambuzi.
Hakimu huyo alisema Mahakama imewahukumu kifungo
cha miaka 30 kwa unyang’anyi wa kutumia silaha na miaka mingine miwili
kwa kosa la kula njama ya kupora fedha hizo.
Hakimu Kobelo aliamuru Dola za Marekani 39,000,
sawa na Sh64 milioni walizokutwa nazo washtakiwa zitaifishwe na Serikali
na zikabidhiwe kwa uongozi wa Benki ya NBC. Hukumu hiyo imekuja wakati
jitihada za Tanzania kuwarejesha nchini, wahalifu watatu kutoka Kenya na
Uganda, wanaodaiwa kuvamia benki hiyo zikiwa zimegonga mwamba.
Watuhumiwa hao ni Patrick Ayis Ingoi, raia wa
Kenya anayedaiwa kuwa kiongozi wa genge la majambazi hao, Charles Lumago
na Shaban Wayabona ambao ni raia wa Uganda.
Hukumu hiyo inafanya idadi ya waliofungwa kwa
uporaji huo kufikia 12, baada ya Watanzania wanne kufungwa kwa kosa
hilohilo Desemba 13, mwaka 2006.
Watanzania hao ni Jackson Ole Nametemi, Benjamin Dia, Kelvin Dia
na Raphael Kalaghe waliofungwa miaka 30 na Evelyne Mlaki na Happy Memei
waliofungwa miaka mitatu.
Mlaki na Memei walitumikia vifungo vyao na
kumaliza wakati washtakiwa wengine walikata rufaa Mahakama Kuu na hukumu
yake haijatolewa kwa miaka mitano sasa.
MWANANCHI
Post a Comment