MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freemon Mbowe, ameshindwa kuhudhuria Mahakamani kutoa ushahidi wake katika kesi inayomkabili, huku wakili wake akishindwa kufika mahakamani hapo.
Mbowe ambeye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, anakabiliwa na mashtaka ya kumshambulia mwangalizi wa ndani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Kesi hiyo iliyoko katika Mahakama ya Wilaya ya Hai, mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Agnes Muhina, imeshindwa kuendelea leo Agosti 18, 2014 ikiwa ni mara ya pili baada ya mtuhumiwa mwenyewe ambaye ni shahidi namba moja, katika kesi hiyo kushindwa kuonekana mahakamani hapo.
Mdhamini aliyemdhamini Mwenyekiti huyo, Awazi Urono, alisema mahakamani hapo kuwa, Mshtakiwa huyo ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kuachwa na ndege aliyokuwa amepanga kusafiri nayo kuja mkoani Kilimanjaro kuhudhuria Kesi hiyo.
“Leo kama dakika mbili zilizopita nimewasiliana na Mbowe, na kunieleza kuwa ameshindwa kufika kutoa ushahidi wake kutokana na ndege aliyokuwa anatakiwa kusafiri nayo kumwacha baada ya kuchelewa kufika uwanjani”alisema Urono.
Upande wa Jamuhuri, unaowakilishwa na Mwendesha mashitaka wa polisi, Inspekta Marwa Mwita, ulidai Mahakamani hapo kuwa taarifa za kutokuwepo kwa mtuhumiwa huyo anayetakiwa kuzisema mahakamani hapo ni wakili wa utetezi na sio mdhamini.
Mwita alisema kuwa pamoja na wakili wa utetezi kushindwa kufika mahakamani hapo bila kutoa sababu zozote za msingi ,anakubaliana na sababu zilizotolewa na kumwomba Hakimu kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya Utetezi.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Septemba 8, mwaka huu ambapo upande wa utetezi unategemea kupandisha mashahidi wawili, akiwemo mshitakiwa mwenyewe.
Ikumbukwe kuwa Julai 17, mwaka huu, kesi hiyo ilishindwa kuendelea kutokana na kile kilichodaiwa na upande wa utetezi kuwa mtuhumiwa huyo ameshindwa kufika mahakani hapo kutokana na gari alilokuwa akisafiri nalo kuelekea uwanja wa ndege ili kuja mkoani Kilimanjaro, kuharibika njiani na kusababisha mtuhumiwa huyo kuachwa na Ndege.
Credit: Mapengo17/jamiiforum



Post a Comment