Aidha,
SADC imemshukuru na kumpongeza aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya
Ukombozi ya Afrika, Brigedia Hashim Mbita wa Tanzania, kwa mchango wake
na uongozi wake wa mapambano ya ukombozi, iwe katika nyanja ya
kuviwezesha vyama vya ukombozi kwa hali na mali, raslimali na ushauri.
Pongezi
hizo kwa Tanzania zilitolewa usiku wa jana, Jumamosi, Agosti 16, 2014,
na Kikao cha Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC – SADC
Troika- kilichofanyika kwenye Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria
Falls, Zimbabwe, chini ya Uenyekiti wa Rais Hifikepunye Phohaba wa
Namibia.
Mkutano
huo wa SADC Troika ulihudhuriwa na wanachama wa Asasi hiyo – nchi za
Namibia, Lesotho na Tanzania. Nchi za Afrika Kusini, Madagascar na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilishiriki kama waalikwa maalum
wa kikao hicho.
Akizungumza
kwenye mkutano huo kwa niaba ya nwenzake, Rais Pohamba
alisema: “Tunawashukuru wananchi wa Tanzania kwa mchango wao wa
kiuchumi, kijeshi na kimkakati katika kuunga mkono kwa hali na mali
jitihada za mapambano ya ukombozi wa nchi zetu.”
Aliongeza
Rais Pohamba: “Sote tunaijua Tanzania, sote tunawajua Watanzania. Kwa
pamoja walitoa jasho na damu na sisi wenyewe katika kutafuta ukombozi wa
nchi zetu. Tutaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wao mkubwa na
usiosahaulika kwa ustawi wa nchi zetu.”
Kuhusu
Mzee Mbita, ambaye Ripoti yake ya shughuli za ukombozi ilitarajiwa
kuwasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC, Rais
Pohamba alisema: “Brigedia Mbita alifanya kazi mchana na usiku
kufanikisha shughuli za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Tunamshukuru sana
kwa uongozi wake na mchango wake mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi
zetu.”
Aliongeza: “Brigedia
Mbita ni raia wa Tanzania na alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya
Ukombozi Kusini mwa Afrika iliyokuwa na makao makuu yake mjini Dar es
Salaam. Alichapa kazi kweli kweli na chini ya uongozi wake, vyama vya
ukombozi vilipata misaada ya hali na mali, misaada ya kiroho na ushauri
wa kijeshi kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa mtu wa shughuli za
jeshi.” Mzee Mbita aliongoza Kamati ya Ukombozi tokea mwaka 1974 hadi
ilipomaliza shughuli zake.
Akizungumza
kwa ufupi sana katika kikao hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimpongeza sana Brigedia
Mbita akisema kuwa alifanya kazi nzuri na kubwa na “tunampogeza kwa kazi
nzuri sana ya kuandaa Ripoti hiyo.”
Ripoti
hiyo inayojulikana kama Mradi wa Hashim Mbita iliongozwa na Meneja wa
Mradi, Profesa Arnold Temu wa Tanzania na imechapishwa na Kampuni ya
Mkuki na Nyota, pia ya Tanzania, ambayo Mtendaji Mkuu wake, Mzee Walter
Bgoya ameandamana na mwakilishi wa Mzee Mbita kwenye mkutano huo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Agosti,2014
|
Post a Comment