Na Baraka Mpenja
MICHUANO ya klabu bingwa Afrika
Mashariki na kati, Kombe la Kagame, imefikia patamu mjini Kigali, Rwanda
ambapo hatua ya robo fainali inaanza kutimua vumbi leo hii.
Mechi ya kwanza itaanza majira ya 9:00 alasiri kwa kuwakutanisha Polisi dhidi ya Atletico, zote za Rwanda.
Robo fainali ya pili itaanza
majira ya saa 11:00 jioni ambapo timu mbili pinzani nchini Rwanda, Rayon
Sport na wanajeshi wa APR wataoneshana kazi.
Kibarua kingine kitaendelea kesho
ambapo mechi iliyotabiriwa kuwa ngumu zaidi katika hatua hii ya kombe
la Kagame itawakutanisha mabingwa wa Tanzania, Azam fc dhidi ya El
Merreikh ya Sudan.
Kutokana na historia nzuri ya El
Merreikh katika soka la Afrika mashariki na kati, hakika Azam
wametumbukia katika daraja zito, lakini kama watajipanga vizuri wanaweza
kuibuka na ushindi.
Meneja wa Azam fc, Jemedari Said
alisema wamejiandaa vizuri na wanafurahia kuchuana na timu ngumu ambayo
itawapa kipimo kizuri cha kujua maendeleo ya kikosi chao.
“Sio pambano jepesi, El Merreik
ni timu yenye historia kubwa. Sisi kama Azam hatuwaogopi, tunawaheshimu,
tutapambana kupata ushindi ili kutinga nusu fainali na hatimaye fainali
na kutwaa ubingwa”. Alisema Jemedari.
Jemedari alisema katika mazoezi
ya jana jioni, wachezaji wote waliokuwa majeruhi, Waziri Salum ambaye
hajacheza mechi yoyote, Saint Prex Lionel, Shomari Salum Kapombe wote
walifanya mazoezi, na kwa mara ya kwanza kikosi kizima kilikuwa uwanjani
kujiandaa na mchezo huo.
Mechi nyingine ya kesho jumatano itawakutanisha KCC ya Uganda dhidi ya Altabara ya Sudan Kusini.
Post a Comment