Watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi wamevamia Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe kilichopo Ushirombo, mkoani Geita na kuua askari wawili na kuiba silaha za moto.
Taarifa za awali za tukio hilo zimethibitishwa na Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, alisema uvamizi huo unatajwa kufanywa
majira ya saa 9 usiku katika kituo hicho mkoani Geita, ambapo inadaiwa
wahalifu hao ambao idadi yao inakadiriwa kuwa zaidi ya kumi, walivamia
kituo wakiwa na silaha za kivita.
Alisema
mazingira ya tukio hilo inaelezwa kuwa majambazi hao walipofika kituoni
hapo, walitupa bomu la mkono katika chumba cha mashitaka na kusababisha
vifo vya askari wawili wenye namba G.2615 Dunstan Kimati na WP 7106
Uria Mwandiga huku wawili wengine wakijeruhiwa.
"Walifika
katika kituo hicho wakiwa na silaha nzito za kivita, wamesababisha vifo
vya askari wawili, lakini wawili wengine wanaendelea na matibabu
hospitalini," alisema Chagonja.
Alisema
baada ya kuwaua na kuwajeruhi askari hao waliharibu taa na kusababisha
giza kutawala kituoni hapo, ambapo walivunja chumba cha kuhifadhia
silaha na kutoweka na baadhi ya silaha.
"Majambazi
hao walivunja na kuchukua baadhi ya silaha ambazo zilikuwepo kituoni
hapo, ambazo mpaka sasa idadi yake haijajulikana," alisema Chagonja.
Chagonja
alisema idadi ya silaha hizo haijajulikana kutokana na operesheni
mbalimbali zilizokuwa zikiendelea wilayani humo, hivyo silaha zilikuwa
zikiingia na kutoka.
Chagonja
alisema, kutokana na tukio hilo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)
Ernest Mangu yuko katika eneo la tukio akiwa amefuatana na Mkurugenzi
wa Upelekezi na Makosa ya Jinai (DCI) Isaya Mngulu na timu ya wataalamu
wa upelelezi na operesheni ili kuhakikisha wahusika wa tukio hilo
wanakamatwa.
Hata
hivyo, aliwataka wananchi kuwa watulivu akisema Jeshi la Polisi
litahakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa na sheria kuchukua
mkondo wake, lakini pia aliwataka wananchi wenye taarifa muhimu
zitakazosaidia kuwakamata wahalifu hao wazitoe ili zifanyiwe kazi.
Kwa
mwaka huu tukio kama hilo la kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi na kuuawa
kwa askari na majambazi kuchukua silaha ni la pili ambapo la kwanza
lilitokea Juni, mwaka huu katika Kituo kidogo cha Polisi cha Mkamba,
wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani ambako majambazi walimuua askari mmoja
na kuwajeruhi wengine watatu na kupora silaha tano zenye risasi ambazo
ni SMG mbili na Shot gun tatu.
Hata hivyo, wahalifu waliohusika na tukio hilo walikamatwa na kesi yao bado inaendelea.
Ingawa
taarifa ya Chagonja haikueleza idadi ya silaha zilizoibwa, taarifa za
ndani ambazo tumezipata zinasema majambazi hao wameiba bunduki kumi,
risasi na mabomu ya mkono, kisha kutokomea.
Imeelezwa
kuwa baada ya kufika kituoni hapo, majambazi hao walizingira kituo
hicho hadi eneo la mapokezi na kuanza kuwamiminia risasi za moto askari
waliokuwa zamu.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dk Honoratha Rutatinisibwa amekiri kupokea miili ya askari wawili wa kike na kiume.
Waliojeruhiwa
wamefahamika kuwa ni askari mwenye namba E.5831 David Ngupama
Mwalugelwa aliyejeruhiwa kichwani na usoni na kwamba ameumizwa vibaya
sehemu za mdomo wake huku meno mawili yaking'oka.
Mwingine ni Mohammed Hassan Kilomo aliyejeruhiwa kifuani na mguu wa kulia uliovunjika mfupa kwa kupigwa risasi.
Dk
Rutatinisibwa alipoulizwa juu ya hali za majeruhi hao, alisema ni mbaya
na kwamba walilazimika kuwahamishia Hospitali ya Rufaa ya Bugando,
jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo awali alithibitisha kutokea
kwa tukio na kuahidi kutoa taarifa zaidi mara baada ya uchunguzi
kukamilika.
Hilo
ni tukio la pili kwa askari wa kituo hicho kuuawa na majambazi ambapo
Juni 28, 2009 kundi la majambazi saba wenye silaha za moto aina ya SMG,
yaliteka magari manne ya mizigo katika pori linalounganisha maeneo ya
Lunzewe, Matabi na Buselesele lililopo Bukombe na kumuua kwa kummiminia
risasi nne kifuani askari Polisi aliyejulikana kwa jina moja la Pascal
wa Kituo hicho cha Polisi Bukombe.
Tukio
hilo la kinyama lilitokea majira ya saa 1:15 asubuhi, ambapo wakitumia
lori lililokuwa limebeba mkaa, waliziba barabara inayokatiza katika pori
hilo wakati Pascal na mwenzake wakisindikiza magari hayo ya mizigo
kupita katika pori hilo.
Post a Comment