Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John
Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuunusuru mchakato wa Katiba Mpya
kwa kulivunja Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.
Aidha, amemtaka Rais kuitisha Bunge la kawaida ili uchaguzi mkuu mwakani uwe huru na haki.
Mnyika alitoa rai hiyo jana jijini
Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana wa
vyama rafiki wa Chadema lengo likiwa ni kuwaandaa kwenye masuala ya
uongozi. Mafunzo hayo ambayo ni mwendelezo wa yale ambayo hutolewa na
Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA), safari hii yamehusisha
vijana kutoka Kenya, Uganda na Tanzania.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo,
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema vijana wa Tanzania na
Uganda wanatakiwa kujifunza kutoka Kenya ambao waliingia kwenye
machafuko baada ya kufanya Uchaguzi Mkuu kabla ya kupata Katiba Mpya.
Alisema matokeo yake viongozi wake
wa juu walifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, (ICC).
Alisema Kikwete anatakiwa atoke kwenye siasa na kuvaa nafasi ya kiongozi
ili kunusuru hayo yaliyotokea Kenya yasijitokeze hapa.
Kuhusu vijana wa nchi za Afrika
Mashariki, Mnyika alitaja changamoto inayowakabili kuwa ni ajira ambayo
aliwataka waliobahatika kupata mafunzo hayo, watoke na mkakati wa
kufanya kampeni ya kupunguza tatizo hilo.
Aliigusia nchi ya Libya na
nyingine duniani ambazo zinapigana vita huku akisema moja ya sababu ya
machafuko ni pamoja na ukosefu wa ajira.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Patrobass Katambi, alisema
wanataka katiba inayokubaliwa na Watanzania wote ambayo itakuwa na tija
kwao.
Kuhusu maandamano ya Chadema
yanayoendelea nchini huku jeshi la polisi likiyazuia kwa kuwakamata,
mwenyekiti huyo alisema matendo ya chama tawala ya kutumia dola vibaya
ndiyo yanayosababisha vurugu na kutokea vita.
Post a Comment