MBUNGE wa Vunjo ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba,
Augustine Mrema (TLP), amesema kuna haja Rais Jakaya Kikwete aongezewe
muda wa kuongoza nchi.
Alisema kama Rais Kikwete ataongezewa muda, atapata muda wa kukamilisha mchakato wa Katiba ambao ndiye aliyeuanzisha.
Mmoja wa wajumbe waliohudhuria kikao kati ya Rais Kikwete na Kituo
cha Demokrasia Tanzania (TCD) kilichofanyika mwanzoni mwa wiki Ikulu
ndogo ya Kilimani mjini Dodoma, aliiambia MTANZANIA kwamba Mrema aliyasema
hayo alipokuwa akichangia wakati wa kikao hicho.
“Wakati mjadala unaendelea, Mrema alipendekeza Rais Kikwete aongezewe
muda wa mwaka mmoja au miwili ili afanikiwe kukamilisha mchakato huu wa
Katiba.
“Alipotoa pendekezo hilo, kuna mjumbe mmoja akamuuliza, ‘sasa Mrema
unataka muda uongezwe ili na wewe upate muda wa kupambana na Mbatia
(James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) anayekusumbua kule Vunjo au?’
“Huyo mjumbe alipouliza hivyo, Mrema akadakia na kusema, ‘hapo hapo’,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa .
Chanzo hicho kilisema kuwa Mrema aliendelea kumsihi Rais Kikwete
amzuie Mbatia asiende Vunjo kwa kuwa anapokuwa huko anatumia jina lake,
kwamba amemtuma kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Mbatia alipozungumza na MTANZANIA kwa simu jana juu ya malalamiko
hayo, alisema hawezi kuendelea kujibizana na Mrema kwa kuwa ni mkubwa
wake.
“Mimi sikulelewa katika mazingira ya kujibizana na wakubwa zangu ila
ninachosema ni kwamba, wakati wa mkutano wangu wa hadhara niliohutubia
Vunjo wiki iliyopita, wenyeviti 11 wa serikali za vijiji walioshinda
kupitia TLP, wenyeviti 32 wa vitongoni ambao ni wa TLP, msaidizi wa
Mrema pamoja na wanachama wapya 1,564, walihamia NCCR-Mageuzi,” alisema
Mbatia.
Naye Mrema alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alikiri kutaka Rais
Kikwete aongezewe muda na kumwomba amzuie Mbatia kwenda Vunjo akidai
kuwa anatumia jina la rais kumsema vibaya kwa wananchi.
Chanzo: Mtanzania
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment