Mtoto Amani Elisha (10) aliyepigwa vibaya na baba yake mzazi hadi kuzimia kwa siku mbili.
KATIKA hali
ambayo siyo ya kawaida iliyowashangaza wakazi wa eneo la Ukonga
Mazizini kwa Makobe, baba mmoja aliyefahamika kwa jina la Elisha Zakari
amedaiwa kumpiga mwanaye wa kumzaa kipigo kama cha ng’ombe machungani na kusababisha azimie na kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.Mtoto
huyo aliyepigwa ni Amani Elisha (10) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya
Msingi Maarifa iliyoko Ukonga, Dar es Salaam, baada ya kipigo alizimia
siku mbili. Tukio
hilo la kikatili lilitokea usiku wa Ijumaa iliyopita na sababu ya mtoto
huyo kupewa kipigo inadaiwa ni kutokana na utoro shuleni na kwamba hata
akienda huwa haandiki.Waandishi wetu waliponasa tukio walimtafuta mama
mzazi wa mwanafunzi huyo maarufu kama mama Amani na mahojiano yakawa
hivi:
Mwandishi: Mama ni kweli kuwa mume wako alimpiga mtoto wenu?
Mama Amani: Ni kweli baba yake Amani ndiye aliyempiga.
Mwandishi: Kwani huyu ni baba yake mzazi?
Mama Amani: Ni baba yake mzazi kweli, wakumzaa.
Mwandishi: Wakati mtoto anapigwa wewe ulikuwepo?
Mama Amani: Hapana,
sikuwepo nyumbani, nilikuwa kwenye shughuli zangu, niliporudi nikakuta
haya. Niliambiwa na majirani kuwa Amani kapigwa na baba yake. Hakukuwa
na jinsi, tulimpeleka mtoto hospitali kutibiwa baada ya kuzimia.
Ilidaiwa kuwa baba
yake aliamua kumpa adhabu mwanaye baada ya kubaini kuwa alikuwa hafiki
shuleni na hata akifika alikuwa haandiki chochote na alipofuatilia,
walimu walimthibitishia.
“Ni kweli huyo baba
aliwahi kufika hapa shuleni akathibitishiwa kuwa mwanaye ni mtoro na
hata akifika ni mvivu kwani haandiki chochote.
“Alipoambiwa hivyo
alipatwa na hasira na kutaka kumchapa hapahapa shuleni lakini
hatukumruhusu. Tulimuambia kama ni kumchapa akafanye hivyo nyumbani
kwake,” alisema mwalimu mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake
gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa shule.
Mtoto Amani Elisha akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
JIRANI ASIMULIA
Jirani
mmoja aliyeshuhudia kichapo hicho aliwaambia waandishi wetu kuwa Elisha
au baba Amani ni jirani yao lakini walishangazwa na kichapo alichokuwa
akimpa mtoto wake.
“Alimpiga kwa muda
mrefu na hakuna hata jirani aliyetoa msaada, kila mtu aliamua kukaa
pembeni huku tukishangaa kipigo alichompa mtoto huyo.
“Mtoto huyo alipigwa
hadi kuzimia lakini baadaye alizinduka na mama yake aliporejea, kwa
kushirikiana na majirani waliamua kumpeleka hospitali,” alisema shuhuda
huyo.
Jirani mwingine ambaye
hakupenda jina lake liandikwe gazetini aliyeongozana na mama huyo
kwenda hospitali, alisema kufuatia hali ya mtoto kuwa mbaya waliambiwa
waende polisi wakachukue PF3 ndipo angetibiwa.
WATINGA POLISI
Baada ya kufika katika
Kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga na kutoa taarifa ya tukio hilo
waliandikiwa PF3 na kumpeleka Amani Hospitali ya Amana kwa ajili ya
matibabu lakini kufuatia hali yake kuwa mbaya alihamishiwa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
AFANYIWA UPASUAJI WA KICHWA
Gazeti hili
lilimfuatilia mtoto huyo katika Hospitali ya Muhimbili na kukuta
amelazwa wodi A, katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi)
akiendelea na matibabu.
“Ni
kweli mtoto huyo anapatiwa matibabu na amefanyiwa upasuaji wa kichwa na
hali yake inaendelea vizuri,” alisema daktari mmoja ambaye hakutaka
jina lake kuandikwa gazetini.
BABA MBARONI
Baba wa Amani anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga, Dar es Salaam huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Gazeti hili linampa pole mtoto Amani na tunamuombea apone haraka ili arejee shuleni kuendelea na masomo pamoja na wenzake.
Post a Comment