KATIKA machapisho ya gazeti hili la Tanzania daima, toleo namba 3554 la Agosti 27, 2014
na toleo namba 3555 la Agosti 28, 2014 tulikuwa na habari zenye vichwa:
Kikwete anywea na Kikwete ‘alamba matapishi’ yake.
Vichwa hivyo vya habari vilileta mkanganyiko mkubwa serikalini, na
Ofisi ya Msajili wa Magazeti, kupitia Idara ya Habari (MAELEZO)
ilitutaka tutoe maelezo, kwa msingi kuwa vichwa hivyo vya habari
vilikuwa vinamdhalilisha Rais.
Tulifafanua maana halisi ya vichwa hivyo na habari zilizoandikwa
lakini ufafanuzi wetu haukumridhisha , msajili na kutaka tuombe radhi
tena.
Tumeona ni jambo la busara zaidi kuomba radhi kwa mara nyingine tena kwakuwa hatukukusudia kumdhalilisha Rais
Kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma na hasa baada ya kubaini
mkanganyiko uliosababishwa na ukali wa maneno ya vichwa hivyo vya
habari, tumeona ni jambo la kiungwana kuomba radhi kwa mara ya pili
katika ukurasa wa mbele habari husika zilipoandikwa.
Na kwa kuwa tumegundua kwamba aliyekwazwa ni Rais mwenyewe,
tumesukumwa na utu na taaluma kumwomba radhi Rais mwenyewe kupitia
gazeti hili.
Habari iliyokuwa na kichwa cha habari: Kikwete anywea, haikulenga
kumdhalilisha au kumshusha hadhi Rais, bali kuelezea kwamba baada ya
mvutano wa muda mrefu kuhusu umuhimu wa yeye kukutana na viongozi wa
Umoja wa katiba ya Wananchi (UKAWA), hatimaye amelegeza msimamo,
amekubali kukutana nao.
Ushahidi ni kwamba vikao hivyo vimekuwa vinaendelea kwa nyakati
tofauti. Ukweli ni kwamba visingefanyika kama rais na washauri wake
wasingelegeza msimamo.
Kuhusu habari iliyosema: Kikwete ‘alamba matapishi yake’, lengo
lilikuwa kusisitiza jinsi Rais Kikwete alivyobadili msimamo ghafla na
kutetea jambo alilowahi kupinga kwa nguvu zote.
Hii ilitokea baada ya Rais Kikwete kusema hadharani kwamba serikali
yake inafikiria kutoa elimu bure, sera ambayo katika uchaguzi wa mwaka
2010 ilikuwa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku yeye
na chama chake wakiibeza.
Tunachukua fursa hii kumuomba radhi Rais pamoja na watu wote
walioguswa kwa namna moja au nyingine na vichwa vya habari vya magazeti
husika.
Post a Comment