Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akifungua mafunzo ya
siku 27 kwa wakufunzi na wadadisi kutoka
Tanzania Bara na Zanzibar watakaoendesha
Utafiti wa Tathmini ya utoaji wa Huduma za Afya nchini 2014/15 leo
mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza na washiriki wa
mafunzo ya Utafiti wa Tathmini ya utoaji
wa Huduma za Afya nchini leo mkoani Kilimanjaro.
Mkufunzi wa
mafunzo ya wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma za
Afya nchini Bi. Saumu Said akiendelea kutoa mafunzo kwa washiriki wa utafiti
huo mkoani Kilimanjaro leo.
Washiriki
wa mafunzo ya Wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma
za Afya nchini wakiendelea na mafunzo yatakayowawezesha kufanya utafiti huo mkoani Kilimanjaro
leo.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akisalimiana
na wakufunzi na wadadisi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watakaoendesha
Utafiti wa Tathmini ya utoaji wa Huduma za Afya nchini 2014/15 walio
kwenye mafunzo leo mkoani Kilimanjaro.
======= ======== =======
SERIKALI YAWATAKA
WASIMAMIZI NA WADADISI WA UTAFITI WA TATHMINI YA HUDUMA ZA AFYA NCHINI
KUZINGATIA WELEDI.
Na. Mwandishi wetu –
Kilimanjaro.
24/9/2014.
SERIKALI imewataka wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Tathmini ya
Utoaji wa huduma za Afya nchini mwaka 2014/15 kuzingatia weledi katika
utekelezaji wa majukumu yao na kuepuka kukusanya
takwimu zisizo wakati wa utafiti huo utakaofanyika nchi nzima kuanzia Oktoba 13
mwaka huu.
Aidha, imewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, madakatari
na wafanyakazi wa vituo
vyote vya kutolea huduma za afya nchini kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaoendesha utafiti huo ili waweze kufika
kwenye vituo vya
kutolea huduma za afya vilivyopo katika maeneo yao kwa lengo la kupata taarifa sahihi zitakazofanikisha utafiti
huo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akizungumza wakati
akifungua mafunzo ya siku 27 kwa wakufunzi na wadadisi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watakaoendesha
utafiti huo amesema kuwa
wakufunzi, wadadisi na wataalam hao
wanayo nafasi kubwa ya kufanikisha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazotoa
taswira halisi ya utoaji wa huduma ya afya nchini kwa mwaka 2014/2015.
Amesema utafiti huo utaiwezesha serikali kutathmini
utekelezaji wa mipango mbalimbali na kufikia malengo iliyojiwekea kitaifa
na kimataifa kwa kuboresha na kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake.
Amesema Serikali imekuwa ikitekeleza programu
mbalimbali za kuboresha huduma za afya na maisha ya Watanzania kwa kupitia Mikakati
ya Kimataifa na Kitaifa ikiwemo ile ya Malengo ya Milenia ya Mwaka 2015 na
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011 -2016).
Amezitaja programu nyingine kuwa ni pamoja ile ya
Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA) na Mkakati wa Kupunguza
Umaskini Zanzibar (MKUZA) kwa upande wa Zanzibar.
Dkt. Seif amesema katika juhudi hizo Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii imekuwa na jukumu la kusimamia programu mbalimbali za afya
na kufuatilia utekelezaji na utoaji wa huduma za afya nchini.
Ameeleza kuwa wakati wa utafiti wa kwanza wa Kutathmini
Utoaji wa Huduma za Afya nchini unafanyika na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka
2006,Tanzania ilikuwa na jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 5669, kati ya hivyo 224 zilikuwa ni
hospitali, 541 vikiwa ni vituo vya afya na
zahanati 4904.
Amesema kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta ya afya hadi kufikia mwaka
2013 ambapo takwimu zinaonyesha kuwepo kwa vituo 6767 vya kutolea
huduma ya afya nchini , hospitali 256, vituo vya
afya 701 na zahanati 5810.
“Nyote ni mashahidi kuwa toka kipindi hicho mpaka sasa
serikali imeendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi wake,sasa tuna huduma ya kuzuia maambukizi
ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto ambayo
inapatikana katika vituo
vyote vinavyotoa huduma za mama mjamzito” Amesisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina
Chuwa akizungumzia mafunzo hayo amesema kuwa washiriki watakaofaulu na kukidhi vigezo
vilivyowekwa watashiriki katika zoezi la kukusanya
takwimu za utafiti huo kwa kipindi cha miezi minne kuanzia tarehe 13 Oktoba 2014 .
Amesema utekelezaji wa utafiti huo na mafunzo hayo unafanywa kwa pamoja na Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii - Tanzania Bara,
Wizara Afya - Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, na Shirika la ICF International la Marekani ambao pia wanatoa ushauri
wa kitaalamu katika kufanikisha utafiti huo.
Dkt. Chuwa amefafanua kuwa utafiti huo utahusisha ukusanyaji wa
takwimu katika sehemu za kutolea huduma za afya kwa lengo la kufahamu utayari wa vituo
vinavyotoa huduma za afya na huduma bora za afya kwa wananchi.
Aidha amezitaja huduma
zitakazoguswa na utafiti huo kuwa ni pamoja pamoja na Huduma za Afya ya Uzazi,
Afya ya Watoto, Maradhi ya Kuambukiza kama vile Kifua Kikuu, UKIMWI, Malaria
pamoja na Maradhi yasiyo ya kuambukiza kama vile magonjwa ya
Kisukari na Moyo.
Amefafanua
kuwa lengo
la kufanyika kwa utafiti huo ni kuiwezesha serikali kujua ni kwa namna gani vituo vinavyotoa huduma ya
afya vimejipanga kutoa huduma bora ya afya kwa kuangalia upatikanaji wa huduma
mbalimbali, vifaa, dawa, miundombinu na rasilimali watu kwa kada mbalimbali.
Kuhusu utafiti huo Dkt. Chuwa amesema ni wa pili kwa ngazi ya kitaifa
ukifuatiwa na ule wa
kwanza uliofanyika mwaka 2006 na
kuongeza kuwa utahusisha sampuli wakilishi ya vituo vya kutolea huduma vya serikali ,binafsi, mashirika ya
umma na vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini ambavyo vimetayarishwa, hospitali maalum zote, hospitali zote za mikoa
, wilaya na baadhi ya vituo vya
afya na zahanati.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro Dkt. Ibrahimu Msengi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo
amesema kuwa
mkoa huo unaendelea
na juhudi za kuboresha huduma za afya zinazotolewa katika vituo vya afya pamoja kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa
Kilimanjaro na kukuza
pato la mkoa huo.
Amesema mkoa umeweka kipaumbele katika
kuboresha miundombinu ya afya iliyopo ili iweze kuakisi ukuaji wa Pato la Mkoa na mahitaji
ya wananchi katika kupata huduma za afya zilizo bora kulingana na ongezeko la
idadi ya Watu.
Amefafanua kuwa utafiti huo umekuja wakati
muafaka ambapo mkoa huo na mikoa mingine nchini inahitaji kuboresha huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma.
Post a Comment