Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inashuka uwanjani Oktoba 12 mwaka
huu kuikabili Benin katika mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mechi
hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili
jioni. Programu ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager kwa ajili ya mechi hiyo itatangazwa baadaye na Kocha Mkuu Mart
Nooij.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na taratibu nyingine kwa
ajili ya mechi hiyo ikiwemo usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu
hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 28.
Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
Wakati
huo huo, kutokana na mechi hiyo ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
inafanyiwa marekebisho madogo, na marekebisho hayo yatatangazwa kesho
(Septemba 26 mwaka huu).
RAIS MALINZI KUFUNGA KOZI YA WANAWAKE
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
anatarajia kufunga mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa vyama vya mpira wa
miguu wa wanawake vya mikoa ya Tanzania Bara.
Hafla
ya kufunga mafunzo hayo itafanyika kesho (Septemba 26 mwaka huu) saa 5
asubuhi kwenye ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mafunzo
hayo ya siku tano yalishirikisha viongozi 34 wakiwemo baadhi ya
waandishi wa habari na Meneja wa Twiga Stars, na yaliendeshwa na
Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Henry
Tandau.
Post a Comment