Wanafunzi
wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya Wilaya ya Tunduru
mkoani Ruvuma wakiwa wamekaa chini na mwalimu wao pembeni kuonesha
sehemu ambayo hutumika kama darasa wawapo masomoni.
WANAFUNZI wa darasa la awali
katika Shule ya Msingi Nakayaya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma
wanasomea chini ya mti kutokana na darasa hilo kuendeshwa bila ya kuwa
na chumba maalum kwa ajili ya kusomea wanafunzi hao.
Hali hiyo imebainika baada ya
mwandishi wa habari hizi kuitembelea shule hiyo hivi karibuni na
kuwakuta wanafunzi wakiwa wamekaa chini huku wakiendelea na masomo hayo
nje chini ya mti ulio na kivuli cha kuwahifadhi wakati wa jua kali.
Akizungumza shuleni hapo Kaimu
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nakayaya, Christina Mhowera alisema
watoto hao wamelazimika kusomea nje baada ya huduma ya elimu hiyo
kuanzishwa shuleni hapo bila ya kuwa na jengo maalum kwa wanafunzi wa
awali.
Alisema awali wanafunzi hao
walikuwa wakisomea kwenye gofu (jengo mbovu) lililokuwa jirani na shule,
lakini walilazimika kuondolewa baada ya jengo hilo kutwaliwa kwa
matumizi mengine. Aliongeza kuwa baada ya hapo walihamishiwa kwenye
nyumba ya mwalimu kabla ya kukamilika lakini waliondolewa tena na kuanza
kusomea nje (chini ya mti) hadi sasa.
Alisema darasa hilo lenye jumla
ya wanafunzi 92 linaendeshwa bila ya kuwa na chumba cha darasa maalum
wala madawati kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa vyumba vya
madarasa hadi hapo watakapopata darasa maalum kwa ajili ya wanafunzi
hao.
Kwa upande wake mwalimu wa
darasa hilo, Teckla Milanzi alisema mbali na darasa hilo kutokuwa na
chumba cha darasa, linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ya uhaba wa
vitendea kazi kama vitabu na vyenzo zingine za kufundishia na hakuna
bajeti yoyote inayotumwa kuliwezesha darasa hilo.
Aidha uchunguzi uliofanywa
katika shule nyingine tatu za Wilaya ya Tunduru, yaani Shule ya Msingi
Nanjoka, Majengo na Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko kuangalia
mazingira ya utoaji elimu ya awali katika shule hizo umebainisha
kukabiliwa na changamoto nyingi hali ambayo inahatarisha msingi wa elimu
kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Msingi Nanjoka, Batadhari Mkwela alisema licha ya usajili wa
wanafunzi wa awali kuongezeka kila mwaka kumekuwa hakuna bajeti ya
kuendesha elimu hiyo.
“…Darasa la awali linahitaji
vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha,
vyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini,
hatuna madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” alisema
Mkwela.
Akizungumzia hali hiyo, Kaimu
Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe alisema vyumba vya madarasa
ni changamoto kubwa eneo hilo licha ya msisitizo kuendelea kutolewa wa
kila shule ya msingi kuwa na darasa la awali. Alisema mwaka 2013/14
halmashauri ya wilaya hiyo ilihitaji zaidi ya milioni 366.7 lakini
ililetewa zaidi ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu tu ya
kiasi kilichopitishwa kwenye bajeti hiyo.
“…Kwa hiyo unaweza kuona kwamba
ni ngumu kuigawa fedha hii katika matumizi maana kwanza haitoshi na pili
hata kilichotegemewa kuja ni pungufu zaidi tena sana, sasa sijui
unaweza kugawa kila shule ipate shilingi ngapi…kwani haitoshelezi,”
Abdul Kazembe.
Akifafanua zaidi Kaimu Ofisa
Elimu huyo alisema miundombinu ya madarasa ni changamoto kubwa, kwani
mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa ni
1,715 lakini madarasa yaliopo ni 900 na kitu huku mengine yakiwa ni ya
muda mrefu na yanaelekea kuchakaa.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
Post a Comment