MWANAUME mmoja aitwaye Amani Mhegere (45) mkazi wa Yombo jijini Dar es Salaam, Julai 18, mwaka huu alinusurika kufa kwa moto baada ya nyumba yake kuanza kuungua akiwa usingizini.Bw. Amani Mhegere (45) aliyenusurika kufa kwa moto baada ya nyumba yake kuanza kuungua akiwa usingizini. Akizungumza na gazeti hili akiwa amelazwa katika wodi namba 23 iliyopo kwenye Jengo la Sewa Haji, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mhegere alisema kama siyo majirani waliouona moto huo na kumwamsha kwa kumwagia maji kupitia dirishani, angekufa.
“Siku hiyo nililala mapema na kupitiwa na usingizi, majira ya saa tatu usiku majirani waliona nyumba niliyolala inaungua moto, walikuja hadi dirishani na kuchungulia, wakaniona nimelala kitandani, walinigongea mlango lakini sikusikia hali iliyowafanya wachukue maji kwenye ndoo na kunimwagia, nikashituka.
“Nilipoona moto nikakurupuka na kukimbilia mlangoni lakini kutokana chumba chote kutanda moshi sikuweza kuuona mlango.
“Kwa kutambua hatari iliyokuwa mbele yangu, nikapata ujasiri, huku nguo niliyokuwa nimevaa ikiwa imeshika moto nilifungua mlango na kufanikiwa kutoka ndani na kwenda kujilaza kwenye mchanga.
“Nikiwa nagalagala chini, majirani zangu walinimwagia maji na kufanikiwa kuuzima.
“Siku hiyo nilikuwa peke yangu, watoto na mke wangu aliyekuwa mjamzito hawakuwepo nyumbani, alikuwa amekwenda kwao Iringa kujifungua.
Muonekano wa karibu wa Bw. Amani Mhegere. Moto huo ulianzia chumbani kwangu baada ya kusahau kuzima mshumaa. Baada ya tukio hilo, majirani walitafuta gari na kunileta hapa hospitalini, kwa kweli ninawashukuru sana kwa ujasiri wao vinginevyo hivi sasa ningekuwa naitwa marehemu.
“Mbali na kunifikisha hapa lakini wamekuwa wakija kunijulia hali jambo linalonifanya nifarijike sana.
“Namshukuru sana mke wangu, kwani baada ya kupata taarifa alikuja kuniona huku akiwa na mtoto wetu aliyejifungua hivi karibuni.
“Ni vigumu kuamini kama leo hii ningekuwa hai kutokana na hali ilivyokua, kwa sasa naendelea vizuri kidogo tofauti na nilivyoletwa, nawashukuru wahudumu na madaktari kwa kunipatia huduma nzuri,” alisema Mhegere.
Post a Comment