JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Rais Jakaya Kikwete
amemteua Bw. Seperatus R. Fella kuwa
Katibu wa Sekretarieti ya Kamati ya Kuzuia Biashara Haramu ya Binadamu.
Kabla ya uteuzi huo,
Bw. Fella alikuwa Kaimu Katibu wa Kamati hiyo
na uteuzi wake unaanzia mwezi Agosti, 2014.
Kamati ya Kuzuia
Biashara Haramu ya Binadamu ilianzishwa chini ya Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu
ya Binadamu ya mwaka 2008 na kazi kubwa ya Kamati hii ni kuzuia na kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji
wa binadamu.
Chimbuko la kutungwa
kwa Sheria ya Kuzuia Biashara haramu ya Usafirishaji wa Binadamu ni Itifaki ya
Kimataifa ya kuzuia, kupambana na kutoa adhabu kwa watekelezaji wa biashara ya
usafirishaji haramu ya binadamu, hasa wanawake na watoto.
Itifaki hii ni
nyongeza ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya uhalifu wa kimataifa wa
kupangwa, ambapo Serikali ya Tanzania imeridhia Mkataba huo na itifaki yake.
Juhudi za Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kushughulikia biashara haramu ya usafirishaji
wa binadamu zinaendana pia na Tamko la
Kimataifa la Haki za Binadamu, Mkataba wa Kimataifa wa kuondoa aina zote za
ubaguzi dhidi ya Wanawake na Mkataba wa Haki za Watoto wa mwaka 1989.
Makosa yanayovunja
Sheria ya kuzuia Usafirishaji haramu wa Binadamu ni pamoja na kupanga,
kupangisha au kutumia nyumba au jengo kwa ajili ya biashara ya usafirishaji wa
binadamu na kughushi hati za Serikali kwa madhumuni ya kukuza biashara ya
binadamu.
Makosa mengine ni
kujipatia pesa kwa kuwatumikisha kwa nguvu watu wazima au watoto wa kike au
kiume katika kufanya kazi za ndani au biashara nyingine haramu kama ngono na
usafirishaji na usambazaji wa madawa ya kulevya, baada ya kuwalaghai au
kuwachukua kwa nguvu kutoka katika makazi yao.
Adhabu kwa wanaotiwa
hatiani kwa kuvunja Sheria hii ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja (1) au
kisichozidi miaka saba (7) au faini isiyopungua shilingi milioni mbili (2) au
kuzidi milioni 50 au vyote kwa pamoja.
Imetolewa na:
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
23
OKTOBA, 2014
Post a Comment