Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Dar es Salaam. Msajili wa
Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) unakabiliwa na changamoto kubwa suala la ruzuku.
Ingawa
hakutaka kuingia kwa undani kuelezea changamoto hiyo, Jaji Mutungi
alisema anaona ugumu wa Ukawa katika kushughulikia tatizo hilo, lakini
akaongeza kuwa wakati ukifika ofisi yake italizungumza.
Alisema
hayo jana alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu uamuzi wa vyama hivyo
vinne kuamua kushirikiana katika chaguzi zijazo na tafsiri yake
kisheria.
Jumapili Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF
vilisaini makubaliano ya kushirikiana katika mambo saba, likiwamo la
kusimamisha mgombea mmoja katika ngazi zote kuanzia chaguzi za serikali
za mitaa hadi Uchaguzi Mkuu ujao.
Jaji Mutungi alisema:
“Maswali hayo unapaswa kuwauliza wao. Tutakuja kuzungumza wakati
ukifika. Suala la ruzuku lina taratibu zake, Muungano una taratibu zake
na ushirikiano pia,” alisema.
“Ruzuku ni changamoto katika suala la Ukawa, lakini sitaki kuingilia hilo kwa kuwa ukifika wakati tutasema.”
Alisema
kwa sasa nchi inaelekea katika uchaguzi, hivyo ni muhimu kwa Ofisi ya
Msajili ikaacha kuingilia hayo. “Lazima niwe careful (makini) katika
mazungumzo yangu, kwani naweza nikawa mimi na wewe (mwandishi)
tunatafsiri sheria, lakini wengine wakafikiria kisiasa,” alisema Jaji
Mutungi.
Kifungu cha 18 cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya
Mwaka 2002 kinaeleza kuwa ruzuku ambazo chama kitapewa zitakuwa ni kwa
ajili ya shughuli za chama husika bungeni, shughuli za kijamii za chama
husika, suala lolote la uchaguzi ambalo chama kimeteua mgombea na kitu
chochote muhimu ambacho chama kitakuwa kinafanya.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa ruzuku ambazo chama kinapata lazima zikaguliwe na kuwasilishwa hesabu kwa Msajili wa Vyama.
Changamoto
hiyo inatokana na ukweli kwamba kuunganisha nguvu kutamaanisha kuwa
chama kitakubaliwa na Ukawa kusimamisha mgombea urais, ndicho
kitakachonufaika na ruzuku, ambayo kwa kiasi kikubwa hutokana na uwingi
wa kura anazopata mgombea wa nafasi hiyo.
Chadema, ambayo
mgombea wake wa urais katika uchaguzi uliopita, Dk Wilbroard Slaa
alipata kura 2,271,941, kinapata ruzuku ya Sh203.6 milioni kwa mwezi,
wakati CUF inapata ruzuku ya Sh117.4 milioni baada ya Profesa Ibrahim
Lipumba kupata kura 695,667.
NCCR-Mageuzi inapata ruzuku ya Sh10 milioni wakati NLD haipati ruzuku yoyote kutokana na kutokuwa na wabunge.
Lakini Dk Slaa anasema ruzuku haikuwa kipaumbele wakati wakifikia makubaliano hayo, bali walitaka kuikomboa nchi.
“Hatukuweka
masilahi yetu mbele na hicho ndicho kitu kinachoisumbua CCM. Sisi
tunachotaka ni kuikomboa Tanzania. Suala la ruzuku na viti maalumu ni
baada ya ukombozi,” alisema Dk Slaa.
“Sisi tunapigania
issues (mambo muhimu), hatupiganii ruzuku wala viti maalumu. CCM ndiyo
wanataka hayo. Sisi tunavipinga hivyo vitu tunavyoona ni kero kwa
Watanzania kwa kuwa viti maalumu havijawahi kuwakomboa Watanzania.”
Dk Slaa alisema wanachotaka ni utawala bora ambao utabadili mfumo uliopo na kuondoa makali ya maisha kwa Watanzania.
“Tuna hasira na kumkomboa Mtanzania na si hizo ruzuku na viti maalumu unavyozungumzia,” alisema Dk Slaa.
Dk
Slaa alisema hata masuala ya nani atagombea urais katika ushirikiano
huo hayana msingi kwa kuwa inawaondoa wananchi kwenye suala la kufikiria
uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umekaribia.
“Mimi nina hasira na kumkomboa Mtanzania, kuwapa elimu bora na mambo mengine muhimu,” alisema Dk Slaa.MWANANCHI
Loading...
Post a Comment