Wiki hii hapa tasnia ya bongofleva ilimpoteza msanii
maarufu YP pichani ambaye anaunda kundi la TMK Wanaume Family.Msanii
huyo ambaye jina lake halisi ni Yessaya Ambikile alifariki usiku
wakuamkia Jumanne katika hospitali ya Temeke.
Said Fella ambaye ni meneja wa kundi hilo amesema kuwa marehemu
alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kifua kwa muda mrefu na ndo kitu
ambacho kimechukua uhai wake.
Historia yake katika muziki:
Saidi Fella anasema kuwa alikutana na marehemu YP kwa mara ya
kwanza mwaka 2004 katika ukumbi wa King Palace huko Temeke.Baadae
kulikuwa na shoo ya TMK Wanaume Family katika ukumbi wa Luxury Pub
marehemu akamfata akaomba amsaidie kimziki, ndipo Fella akamwambia
amwimbie, akamwimbia wimbo wake uliokuwa unaitwa ‘Saidali’ na huo ndo
ukawa mwanzo wakuitwa kwenye kundi hilo.
Alivyofika kwenye kundi baada ya kumwambia Juma Nature kuhusu
kipaji cha marehemu, Nature akamwambia kama yeye Fella ameona marehemu
ana uwezo basi ni sawa apewe nafasi katika kundi hilo.
Mwaka 2005 marehemu pamoja na msanii mwingine wa kundi hilo Y Dash
akatoa wimbo wao wa kwanza ‘Shemsa’ ambao ulifanya vizuri na
kumtambulisha msanii huyo kwenye tasnia ya muziki.Kutokana na sauti ya
marehemu kuendana na msanii mwenzake Y Dash wakatoa wimbo mwingine
uliokuwa unaenda kwa jina la ‘Pumzika’.Said Fella aliendelea kueleza
kuwa marehemu alitoa wimbo ulioenda kwa jina la ‘Mapengo matatu’ ambao
ni wimbo alioimba kutokana na kufiwa na baba yake,mama yake na mdogo
wake.Mwaka 2006 marehemu pamoja na Y Dash ambaye kwasasa yuko nchini
Afrika Kusini wakatoa album ya pamoja waliyoipa jina la ‘Mapengo
matatu’.
Baada ya hapo marehemu akaendelea kushiriki kwenye kazi zingine za
wasanii wa kundi la Tmk Wanaume Family na kazi za kundi kama ‘Twende
zetu’ , ‘Dar mpaka Moro’, ‘Kichwa kinauma’ na nyingine nyingi.
Mwaka 2008 marehemu aliamua kuondoka katika kundi hilo na msanii
mwenzake Y Dash pamoja na Jebby wakaenda kundi lingine ambalo walilipa
jina la TMK Unity.Said Fella anasema mwaka 2010 msanii huyo alimtafuta
nakumuomba kurudi katika nafasi yake tena ndipo alipomkubalia nakuwa
kwenye kundi hilo mpaka kifo chake.Baada yakurudi TMK Wanaume Family
nyimbo ambazo alizoshiriki marehemu nakufanya vizuri ni ‘Kichwa
kinauma’, ‘Tunafurahi’ ya Mh Temba na Chegge.
Meneja huyo wa kundi hilo anasema kuwa kundi hilo limepata pengo
kwasababu toka mwanzo kabla wakati TMK Wanaume Family kuvunjika msanii
huyo alikuwa ni kati ya wale wasanii 11 wa mwanzo.Said Fella alifanunua
kuwa alikuwa akianza Juma Nature,Chegge,Kr,Mh Temba na wengine na yeye
YP anakuwa na namba.Kitu kingine alisema kuwa watamkumbuka YP kwa
ucheshi na ubunifu wa staili za kucheza. “Yaani zile staili zote za TMK
Wanaume Family kama mapangashaa nyingi alikuwa akizibuni marehemu pamoja
na Kr, alikuwa ni mtu anayependa kucheza, mtu wakutengeza step”, Said
Fella.Alieleza kuwa kazi ya mwisho ya kundi marehemu kurekodi ilikuwa ni
mwezi uliopita katika studio za Sound Crafters.
Marehemu,Mh Temba na Chegge
Pia msanii wa kundi hilo Chegge alimzungumzia marehemu nakusema
kuwa alipatwa na uchungu hadi anajikuta analia kwasababu watu wengi
walikuwa wakizifananisha sauti zao na ndo maana alipenda kumshirikisha
kwenye nyimbo zake.Msanii mwingine wa kundi hilo Mh Temba alisema kuwa
atakumbuka ucheshi wa marehemu na pia ubunifu wake katika kutunga
viiitikio(chorus) za nyimbo. “Kwakweli TMK Waunaume Family tumepoteza
jembe.
Marehemu Yessaya Ambikile alizikwa jana katika makaburi ya
Chang’ombe Maduka mawili alizaliwa tarehe 10 November mwaka 1986 jijini
Dar es salaam akiwa ni mtoto wa kwanza, kisha akapata elimu ya msingi
katika shule ya msingi Keko Magurumbasi.Baada yakumaliza elimu ya msingi
marehemu hakuendelea na masomo akaanza kujishughulisha na muziki mpaka
kifo chake.Marehemu ameacha mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka 8
pamoja na mzazi mwenzake ambaye alikuwa ana mpango wakufunga ndoa
hivikaribuni.
Mungu ampuzimshe kwa amani YP.
Post a Comment