Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China leo, Alhamisi, Oktoba 23, 2014, zimetiliana saini Hati za Makubaliano (Memorandum of Undestanding) ambako taasisi za China zitawekeza mabilioni ya dola za Marekani katika uchumi wa Tanzania.
Shughuli hiyo ya utiaji saini imekuwa sehemu ya Mkutano wa Tatu wa Uwekezaji Kati ya Tanzania na China uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya Diaoyutai mjini Beijing, China.
Aidha, utiaji saini huo ambao utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya Kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping. Rais Kikwete ameshuhudia shughuli hiyo ya utiaji saini.
Miongoni mwa Makubaliano yaliyotiwa saini ni pamoja na Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na Kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) ambako kiasi cha dola bilioni moja unusu zitawekezwa katika uchumi wa Tanzania.
Miongoni mwa Makubaliano yaliyotiwa saini ni pamoja na Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na Kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) ambako kiasi cha dola bilioni moja unusu zitawekezwa katika uchumi wa Tanzania.
Kiasi cha dola bilioni moja zitawekezwa katika ujenzi wa mji mpya wa Salama Creek Satellite, eneo la Uvumba, Wilaya yaTemeke, Dar es Salaam na kiasi cha dola 500 zitawekezwa katika ujenzi wa Financial Square, eneo la Upanga.
Aidha, NHC itapata kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kutoka Kampuni ya Poly Technologies kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Valhalla, eneo la Masaki, Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limetiliana saini Makubaliano na Kampuni ya Hengyang Transformer ambako Kampuni hiyo ya Tanzania itapata mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ta mradi wa kusambaza umeme vijijini.
Aidha, Shirika hilo la TANESCO limetiliana saini Makubaliano ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Kinyerezi IV.
Halmashauri ya Manispaaa ya Temeke, Dar es Salaam imetiliana saini Makubaliano na Kampuni ya Jiangyin Tianhe Gasses Group ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kikwete Friendship Highway katika Wilaya ya Temeke. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Saidi Mecky Sadiq na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mheshimiwa Sofia Mjema wameshuhudia utiaji saini Makubaliano hayo.
Vile vile, Mkoa wa Pwani, umetiliana saini Makubaliano na Kampuni ya Jiansu Shenli Plastics Gropu Limited ya China kwa ajili ya kugharimia na kuendeleza Mradi wa Viwanda na Uchumi katika eneo la Mlandizi. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mama Mwantumu Bakari Mahiza ametia saini kwa niaba ya Mkoa wake.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
23 Oktoba,2014
Post a Comment