Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Dk. Abdirahman Duale Beyle amesema kuwa, balozi za Somalia nje ya nchi zimepunguzwa na kufikia 31 kote ulimwenguni.
Duale amesema kuwa, balozi hizo zimepungua tangu kulipofungwa balozi tisa za nchi hiyo barani Afrika, Mashariki ya Kati, Asia na hata Ulaya. Ofisi hizo za uwakilishi wa kisiasa zilifungwa kwa muda kufuatia kuongezeka gharama za uendeshaji wake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia amesema kuwa serikali ya Mogadishu imekwishachunguza sababu zilizopelekea kufungwa balozi hizo tisa na kubaini kwamba suala hilo halitaathiri uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na nchi husika zilikofungwa balozi hizo. Amesisitiza kwamba hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na matatizo ya kifedha na si kwa sababu nyenginezo.
Amezitaja nchi hizo kulikofungwa balozi za Somalia kuwa ni pamoja na Tanzania, Burundi, Syria, Ujerumani, Uingereza, Malaysia, Libya, Rwanda na Sudan Kusini.
Post a Comment