Chama
cha Mapinduzi kimepokea kwa furaha matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika
nchini Msumbiji tarehe 15 Oktoba 2014. Chama Cha Mapinduzi kilikuwa
kinafuatilia kwa karibu mchakato wote wa Uchaguzi huo hasa kwa sababu
Tanzania na Msumbiji ni nchi zenye uhusiano wa damu.
Kilifuatilia
kwa karibu kwa kuwa pia CCM na Chama cha FRELIMO ni vyama ndugu vyenye
historia moja na ya pamoja ya Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Historia
hiyo ndiyo iliyomfanya Rais Mteule wa nchi hiyo Ndugu Filipe NYUSI mara
baada ya kuteuliwa kwake na FRELIMO kugombea Urais, nchi ya kwanza
kuitembelea kuwa Tanzania.
Ikumbukwe
kwamba huyu si mgeni hapa Tanzania. Kama wanaharakati wengine wa
ukombozi, Ndugu NYUSI aliishi Tanzania, anaongea vizuri Kiswahili na
anaichukulia Tanzania ni nyumbani.
Kwa
mnasaba huo, Chama Cha Mapinduzi na Watanzania kwa ujumla tuna kila
sababu ya kushangilia ushindi walioupata ndugu zetu wa FRELIMO, kwani
ushindi wao ni ushindi wetu.
Tunampongeza
sana Rais Mteule Filipe NYUSI kwa kupeperusha vema bendera ya FRELIMO.
Matokeo ya Uchaguzi yamedhihirisha imani kubwa waliyonayo wana-Msumbiji
kwa FRELIMO na kwa Rais Mteule Filipe NYUSI.
Tuna
imani kwamba chini ya uongozi imara wa Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, na Rais Mteule Filipe NYUSI, uhusiano kati ya vyama
vyetu viwili utaimarika na kustawi.
Tunampongeza
pia Rais Armando GUEBUZA kwa kuiongoza FRELIMO na Taifa lake vema na
kukamilisha uongozi wake kwa mafanikio makubwa. Tunamtakia maisha tulivu
ya kiongozi huyo mstaafu.
Anapoanza
kipindi hiki cha uongozi wa Taifa lake, sisi wana-CCM tunamtakia Ndugu
NYUSI afya njema, busara, maarifa na uongozi uliotukuka.
CCM
itasimama pamoja na FRELIMO katika kuendeleza urithi ulioachwa na
waasisi wa vyama vyetu Mwalimu Julius NYERERE na Ndugu Samora MACHEL.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI
31/10/2014
Post a Comment