Licha
ya kutoa ajira kwa maelfu ya vijana wa Kitanzania na pia kupunguza
tatizo la usafiri mijini litokanalo na foleni, usafiri wa pikipiki
maarufu kama 'bodaboda' umeendelea kuua watu kimyakimya na
kuwasababishia ulemavu wa kudumu maelfu ya manusura wa ajali za vyombo
hivyo kila uchao.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa mbali na vifo na ulemavu, bodaboda
zimeathiri pia utoaji wa huduma katika hospitali zinazopokea majeruhi wa
vyombo hivyo, kwani wodi zimefurika kupita kiasi na kusababisha
wagonjwa wengi kulala chini.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga,
ameiambia NIPASHE kuwa katika kipindi cha mwaka 2013 peke yake, pikipiki
8,241 zilihusika katika ajali 6,831 na kusababisha vifo vya watu 1,098
na kuwajeruhi wengine 6,578; huku baadhi yao wakiishia kupata ulemavu wa
kudumu. Idadi hiyo ni sawa na wastani wa vifo vya watu watatu kila
uchao na majeruhi 18.
DAR, MORO, PWANI VINARA
Akieleza zaidi, Kamanda Mpinga anasema kwa kipindi cha kuanzia Januari
hadi Agosti mwaka huu, pikipiki 3,998 zilihusika kwenye ajali 3,777 na
kusababisha vifo vya watu 608 na majeruhi 2,883.
Aidha, takwimu za mikoa zinaonyesha kuwa jiji la Dar es Salaam ndilo
linaloongoza kwa kuwa na matukio ya ajali za bodaboda. Mwaka jana,
bodaboda 3,970 zilihusika katika ajali 3,405 jijini Dar es Salaam na
kusababisha vifo vya watu 172 na majeruhi 3,541.
Kadhalika, katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, jiji la Dar
es Salaam lilikuwa na ajali 1,687 zilizohusisha pikipiki 2,280 na
kusababisha vifo vya watu 113 na majeruhi 1,539.
Kamanda Mpinga anasema mkoa unaoshika nafasi ya pili kwa ajali za
bodaboda ni Morogoro; uliokuwa na ajali 657 na kuhusisha pikipiki 866
zilizosababisha vifo 73 na majeruhi 557 kwa mwaka 2013
Mwaka huu, kwa kipindi cha Januari hadi Agosti, Morogoro kulikuwa na
ajali 191 zilizohusisha pikipiki 264 na kusababisha vifo vya watu 41 na
majeruhi 202.
Mpinga anautaja mkoa unaoshika nafasi ya tatu kuwa ni Pwani, wenye
matukio 428 ya ajali zilizohusisha pikipiki 589, vifo vya watu 84 na
majeruhi 466 kwa mwaka 2013, huku kwa kipindi cha Januari hadi Agosti
mwaka huu mkoa huo ukiwa na matukio 121 yaliyohusisha pikipiki 164 na
kusababisha vifo vya watu 40 na majeruhi 172.
Kilimanjaro unashikilia nafasi ya nne katika janga hilo. Ulikuwa na
ajali 372 zilizohusisha pikipiki 409 na kusababisha vifo vya watu 74 na
majeruhi 343 kwa mwaka 2013. Kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, mkoa
huo ulikuwa na ajali 104 zilizohusisha pikipiki 121 na kusababisha vifo
vya watu 22 na majeruhi 88.
Mikoa mingine na idadi ya ajali za bodaboda katika kipindi cha mwaka
2013 kwenye mabano ni Ruvuma (213), Katavi (190), Arusha (180), Manyara
(154), Tabora (128), Dodoma (123), Rukwa (110), Mwanza (96), Mbeya
(90), Kigoma ( 82), Shinyanga (81) na Kanda Maalum ya Tarime/Rorya ajali
80.
Mingine ni Mtwara (77), Lindi (59), Singida (54), Geita (50), Kagera
(43), Mara (42), Tanga (35), Njombe (27) na Simiyu ikiwa na matukio
machache zaidi ya ajali za bodaboda yaliyoripotiwa Polisi baada ya
kukumbwa na ajali 18 katika kipindi chote cha mwaka 2013.
Akielezea kuhusu hatua zitakazosaidia kupunguza zaidi ajali za bodaboda
nchini, Mpinga anasema elimu ndiyo nguzo ya kumaliza ajali za bodaboda
na kwamba tangu mwaka 2010, wamekuwa wakitoa elimu na wanaamini kuwa
walau kiwango cha ajali za bodaboda kimekuwa kikipungua.
Kamanda Mpinga anasema katika utafiti wao, wamebaini vyanzo vya ajali
nyingi ni makosa ya kibinadamu ambayo ni pamoja na kutoheshimu sheria,
mwendo wa kasi, ulevi wa madereva (ukiwamo wa unywaji wa viroba kabla ya
kuendesha), pikipiki kupakiza abiria wengi zaidi ya uwezo wake maarufu
kama mishkaki na madereva kutokuwa na leseni zinazothibitisha kuwa na
uwezo wa kutumia vyombo hivyo vya moto.
Anataja vyanzo vingine kuwa ni ubovu wa miundombinu kama mashimo,
utelezi na kona kali barabarani na watumiaji kutovaa kofia ngumu
(helmet) huchangia kuongeza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za
pikipiki.
REKODI YAWEKWA MOI
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi)
peke yake hupokea wastani wa majeruhi 77 kwa wiki wanaotokana na ajali
za bodaboda, hiyo ikiwa ni sawa na wastani wa majeruhi 11 kwa siku.
Dk. Mwanga Joseph wa Moi anasema asilimia 55 ya majeruhi wote
wanaofikishwa kwao kutokana na matukio ya ajali jijini Dar es Salaam
huwa ni kutokana na bodaboda.
Anasema wingi huo wa majeruhi wa bodaboda husababisha mrundikano wa
wagonjwa wodini kiasi cha kuzidi idadi ya vitanda na hivyo wengi
hulazimika kulala chini.Anasema licha ya changamoto zilizopo sasa, wao
wanaendelea kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma na wanaamini kuwa
ufumbuzi wa tatizo la mrundikano uliopo sasa Muhimbili ni kuwa na matawi
zaidi ya Moi kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya ili kupunguza idadi ya
wagonjwa wanaofikishwa hapo kila uchao.
Msemaji wa Moi, Patrick Mvungi, anasema kwa mwezi mmoja, wagonjwa wa
ajali ni 600 na kati yao, 330 sawa na asilimia 55, ni wa ajali za
bodaboda.
Mvungi anasema kuwa licha ya majeruhi wa pikipiki kuwa wengi kiasi cha
kuzidi uwezo wa wodi zao, bado wanapowapokea huwachukulia kuwa ni sawa
na majeruhi wengine na wala hawawatengi kwenye wodi maalum kama ambavyo
imekuwa ikivumishwa na baadhi ya watu.
" Kuna uvumi kuwa (Moi) tumetenga wodi kwa ajili ya majeruhi wa ajali za
pikipiki... (hili) siyo kweli. Hata viongozi wa waendesha pikipiki wa
Temeke kupitia umoja wao walishafika kuuliza hilo, tukawahakikishia
kwamba majeruhi wote wanalazwa kwenye wodi moja bila kubaguliwa na hivyo
hakuna sehemu maalum kwa ajili yao," alisema.
Akieleza zaidi, Mvungi anasema kuwa kwa ujumla hali siyo nzuri kutokana
na msongamano wa wagonjwa unaotokana na ajali nyingi za bodaboda.
"Wodi ina uwezo wa kulaza wagonjwa 33 kwa maana ya vitanda vilivyopo,
lakini wagonjwa huongezeka na kufikia 90. Hali hii siyo nzuri.
Tunalazimika kuweka magodoro chini na kuwapa huduma kwa sababu sisi ni
hospitali ya umma, hatuwezi kumkataa mgonjwa anapofikishwa (kwetu) akiwa
katika hali yoyote ile," anasema.
Mvungi anasema kuwa mbali na mipango mingine kadhaa waliyo nayo, lakini
njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto ya mrundikano wa wagonjwa
kwenye wodi zao ni kukamilika kwa jengo la ghorofa saba hivi karibuni
litakalokuwa na vitanda 380 na vifaa vingine vingi vya kisasa.
"Licha ya hali ngumu iliyopo sasa, (sisi) tunaendelea kuwa taasisi bora inayotoa huduma kwa wagonjwa," anasema.
"Ndani ya jengo hilo tutaboresha zaidi kwa kuwa tunatumia mfumo wa
kompyuta na kuachana na mafaili (ya makaratasi) katika kuhifadhi taarifa
za mgonjwa. Madaktari watakuwa na uwezo wa kuwasiliana na wenzao
waliopo nje katika uboreshaji wa huduma za afya," anasema na kuongeza
kuwa taasisi yao imetunukiwa cheti cha ubora Afrika Mashariki.
GHARAMA BADO NAFUU
Mvungi anasema gharama za upasuaji ni Sh. 200,000 na za kupokewa kwa
huduma za awali ni Sh. 50,000, hiyo ikiwa ni nusu ya gharama halisi.
Anasema katika ajali nyingi za bodaboda, majeruhi huvunjika mfupa mrefu
wa mguu ambao hutakiwa kuwekwa vifaa maalum vinavyouzwa nje ya nchi kwa
dola 300 za Marekani (Sh. 480,000).
Anasema kwa ujumla, gharama anazolipa mgonjwa ni ndogo kwa kuwa
serikali hutoa ruzuku na kwamba, kwa kawaida huwa kuna wagonjwa wa aina
mbili; ambao ni wanaolipiwa na Moi baada ya kushindwa kumudu na wengine
wanaojilipia wenyewe.
MAJERUHI KUTELEKEZWA WODINI
Anaongeza kuwa majeruhi wengi wa bodaboda hawana uwezo wa kumudu gharama
za matibabu na kwamba umoja wao (waendesha bodaboda) huonekana siku
wanayoletwa hospitalini, lakini baadaye wenzao wote hupotea na mgonjwa
kukosa wa kumhudumia, labda itokee bahati mbaya kwamba mgonjwa apoteze
maisha na ndipo hapo waliomleta na kumsaidia katika siku za awali
huonekana tena.
"Wengi wa vijana hawa ni wale ambao wanategemea bodaboda kwa ajili ya
kujipatia kipato. Wengine ni za kwao na wengine za matajiri... hawa,
wengi hutelekezwa na Moi hulazimika kuwagharimia," anasema Mvungi.
Mvungi anaelezea changamoto nyingine kuwa ni kutelekezwa hospitali kwa
majeruhi wa bodaboda. Anasema kundi la waendesha pikipiki au watembea
kwa miguu huokotwa kama wagonjwa wasiofahamika na kwamba wanapofikishwa
kwao, hutibiwa kwa matarajio kuwa wakizinduka ndugu zao watajitokeza au
wakipona watalipia gharama wenyewe; lakini kwa baadhi yao hali huwa
tofauti kwani hushindwa kulipia kutokana na vipato vyao kuwa duni.
"Ni mzigo kwa taasisi kumlisha mgonjwa, kumtunza na kumuwekea vifaa
maalum ili arejee katika hali yake ya kawaida. Lakini kupitia sera ya
msamaha wa matibabu, wagonjwa wa aina hii huwa wanasamehewa," anasema na
kuwashauri madereva wa bodaboda kujiunga na bima ya afya ili wanapopata
ajali au kuugua iwe rahisi zaidi kwao kupata matibabu.
MTAALAM WA USAFIRISHAJI ANENA
Mkufunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Injinia Hans Mwaipopo, anasema
vyanzo vya ajali ni vitatu ambavyo ni binadamu anayechangia kwa asilimia
76, chombo anachotumia asilimia 16 na mazingira asilimia nane.
Anasema binadamu anachangi kwa asilimia hiyo kutokana na ukosefu wa
elimu ya usalama barabarani kwa vile wengi hawajui sheria zinazowaongoza
wawapo barabarani.
Mwaipopo anasema pia tabia ya kupuuza sheria kwa wanaofahamu huchangia
ongezeko la ajali; kuporomoka kwa maadili kwani sasa ni rahisi mtu
kupata cheti kwamba amesomea na kukionyesha hata kama hajawahi kusomea
udereva.
Aidha, Mwaipopo anaongeza kuwa lipo pia tatizo la watu kupewa vyombo
vya moto bila kujihakikishia kuwa ni wazima kiakili kwani upo uwezekano
kwa watu wenye matatizo ya akili kuendesha vyombo vya moto kama pikipiki
na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia.
Mkufunzi huyo anasema katika nchi nyingi zilizoendelea, kabla ya mtu
kukabidhiwa leseni anapimwa akili na hilo pia linapaswa kuzingatiwa ili
kupunguza ajali.
Mwaipopo anasema sheria namba 30 ya 1973 na marekebisho yake inasema
dereva mwenye leseni halali anatakiwa kuwa na sifa kuu tatu, ambazo ni
pamoja na kusomea udereva katika chuo kilichosajiliwa na chenye walimu
na macho yake yawe yanaona vizuri.
Sifa nyingine ni kutokuwa na ulemavu unaoweza kuathiri chombo cha moto
anachoendesha, kuwa na akili timamu, awe na afya njema na asiwe na
maradhi yenye kuathiri chombo anachoendesha kama ugonjwa wa moyo, sukari
na kifafa.
" Leo hii wapo madereva wana matatizo ya kifafa. Tukifanya ukaguzi,
tutabaini kwamba wapo wengi wana matatizo ya macho, kifafa, moyo na
sukari lakini wanaendesha vyombo vya moto. Hii ni hatari," anasema.
Anasema chombo kinachangia kwa asilimia 16 kwa maana ya matumizi mabaya,
ikiwa ni pamoja na chombo kwisha muda wake wa matumizi, lakini bado
kinaendelea kubaki barabarani.
Anasema mazingira yanachangia kwa asilimia nane, ikitokana na
miundombinu mibovu na kukosekana kwa alama muhimu katika barabara na pia
barabara kulazimishwa kona pasipostahili na nyingi kujengwa chini ya
kiwango.
Anasema changamoto iliyopo kwa watu wa bodaboda, ni tabia ya wengi wao
kufundishana wao kwa wao. Hawajifunzi sheria za usalama barabarani na
hivyo hujiona wenye haki kuliko watumiaji wengine.
"Mara kwa mara huwa tunawaona... mtu anatakiwa kupita kushoto, yeye
anapita kulia na hawana kofia ngumu... katika hili hatuwezi kutafuta
mchawi, ni lazima ajali zitaendelea kutokea na vifo na majeruhi
kuongezeka," anasema.
AJIRA NA FOLENI
Bodaboda zimekuwa zikisaidia kupunguza tatizo la usafiri katika maeneo
mengi nchini. Katika maeneo ya mijini kama Dar es Salaam ambako tatizo
la foleni limekosa suluhu ya haraka, bodaboda ndiyo kimbilio.
Kwenye maeneo yasiyofikika kirahisi kwa usafiri wa gari, hasa vijijini,
bodaboda pia zimetwaa nafasi. Vyombo hivi ni mkombozi pia wa
Watanzania, hasa vijana wanaokabiliwa na tatizo la ajira.
Dereva Sudi Hassan wa Mbagala Charambe anasema kuwa kwa wastani, kila
siku huwa hakosi kuingiza Sh. 20,000, sawa na Sh. 600,000 kwa mwezi na
kiasi hiki ni kikubwa mno kulinganisha na wastani wa pato la Mtanzania
kwa mwaka (2013) ambalo ni Sh. 1,186,424, sawa na Sh. 98, 868.67 kwa
mwezi, au Sh. 3,295.62 kwa siku; hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa ya
serikali iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwenye Mkutano Mkuu wa
30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) uliofanyika jijini Tanga Mei
14, 2014.
Hata hivyo, vifo vya ajali za vyombo hivi vinavyosababisha kuongezeka
kwa idadi ya wajane na watoto yatima nchini huhalalisha hisia kwamba
pamoja na faida zake, bodaboda ni "muuaji wa kimyakimya".
Ajali za bodaboda zimekuwa zikichangia ongezeko la yatima. Takwimu
zilizowahi kutolewa mwaka 2011 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto, zilionyesha kuwa Tanzania ilikuwa na watoto
yatima milioni 2.4 hadi kufikia mwaka 2011; kati yao wasichana wakiwa
1,055,000 na wavulana 1,345,000.
Aidha, ajali za bodaboda zinaathiri uchumi wa watu mmoja mmoja na taifa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga, idadi ya pikipiki zilizohusika katika
ajali mwaka 2013 peke yake ni 8,241. Hivyo, ikiwa kila pikipiki
hununuliwa kwa wastani wa Sh. milioni 2 na kisha kuharibika kabisa baada
ya kupata ajali, maana yake jumla ya Sh. bilioni 16.48 zilipotea katika
kipindi cha mwaka 2013.
Kadhalika, vipato vya watu wanaotegemea pikipiki hizo kwa shughuli za
kibiashara viliathirika kwa kiasi kikubwa kwani, kama kila dereva wa
bodaboda alitarajia kuingiza wastani wa Sh. 600,000 kwa mwezi (kama
ilivyo kwa dereva Hassan wa Mbagala Charambe), maana yake ni kwamba pato
la jumla ya Sh. 7,200,000 lilipotea kwa kila pikipiki kwa mwaka 2013.
Hivyo, kwa taifa zima (pikipiki 8,242), kiasi kilichopotea kutokana na
bodaboda zilizohusika katika ajali ni Sh. bilioni 4.94. Kwa makadirio ya
jumla, hasara iliyotokana na gharama za kuharibika kwa pikipiki hizo
pamoja na kipato kilichopotea kwa kutokuwapo barabarani kwa pikipiki
hizo kwa mwaka wa 2013 ni takriban Sh. bilioni 21.
UZOEFU WA UGANDA
Changamoto zitokanazo na ajali za bodaboda zipo pia katika nchi
nyingine za Afrika, Mashariki. Kwa mfano, nchini Uganda, mwaka 2011
pekee, madereva wa bodaboda 570 walifariki dunia. Wodi ya dharura katika
Hospitali ya Rufaa ya Mulago jijini Kampala imepachikwa jina la
"bodaboda" kutokana na kuwa na majeruhi wengi wa ajali za bodaboda.
Hospitali hii peke yake, kwa mwaka hupokea wastani wa majeruhi 7,280,
sawa na majeruhi 20 kwa siku.
KAULI ZA MADEREVA
Frank Chungu aliyefanya kazi ya kuendesha pikipiki kwa miaka mitano
katika kijiwe cha Mwenge jijini Dar es Salaam anasema chanzo cha ajali
nyingi za bodaboda ni matumizi ya vilevi kama bangi na pombe kali za
kwenye vipakiti ambayo hutumiwa na waendesha pikipiki wengi.
Anasema wengine hujifunza kwa muda mfupi na kuingia barabarani kama
madereva kamili na matokeo yake, wengi kati ya hao hawafuati sheria za
usalama barabarani na kujiweka katika hatari kubwa ya kupata ajali.
"Wengi hawaheshimu taa za barabarani, Wanapita upande ambao siyo
sahihi. Hawako makini, wanatumia pombe … na kuvuta bangi. Kwa hali kama
hii ni lazima kutakuwa na ongezeko la ajali," anasema.
Chungu anasema hivi sasa walau kuna mabadiliko kidogo ukilinganisha na
miaka michache iliyopita hasa kutokana na wengi wa madereva kuingiwa
woga baada ya kushuhudia wenzao wengi wanavyojeruhiwa na kupata ulemavu
wa kudumu na wengine kupoteza maisha huku wakiacha wake na watoto zao.
Kuhusu leseni, anasema kwa sasa wengi wao wana leseni, lakini tatizo ni
kwamba, hawajifunzi kwa umakini kwani wapo wanaokwenda kujifunza
uwanjani siku ya kwanza na ya pili yake wanaingia barabarani kupakia
abiria.
Anasema wengine huendesha kwa kasi kubwa kwa sababu tu ya kutaka
wasifiwe kuwa wao ni mahiri na kwa bahati mbaya, kadri pikipiki
inavyozidishwa mwendo ndivyo inavyokuwa nyepesi kuiendesha na hivyo
dereva kusahau kuwa tofauti na gari, wao wakipata ajali ni miili yao
ndiyo hujigonga na hivyo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza
maisha au kuwa walemavu.
NINI CHA KUFANYA
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mpinga, anasema kwa
mujibu wa sheria ya usalama barabarani, sura ya 168 kama iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002, mtu yeyote, ili apate leseni ni lazima kwanza
apate mafunzo kwenye vyuo vya udereva.
Kuhusu madereva pikipiki anasema Chuo cha Ufundi Stadi (Veta),
wanaendesha programu ya mafunzo kwa madereva pikipiki, lakini
kinachosikitisha wengi hawapendi kwenda kujifunza.
Anasema wengine wanaotoa mafunzo ni wadau mbalimbali wa masuala ya
usalama barabarani ambao hupita kwenye maeneo ya vijiwe vya madereva wa
bodaboda kwa ajili ya kufundisha matumizi ya pikipiki yanayozingatia
usalama wa waendeshaji wa vyombo hivyo na abiria wao.
Kutokana na kasi ya utoaji wa mafunzo kwa sasa, kati ya waendesha
pikipiki 700,000 waliopo nchini kote, asilimia 70 tayari wamepata
leseni.
Injinia Mwaipopo anasema ni lazima serikali ichukue hatua madhubuti za
kuwafundisha waendesha pikipiki wote ambao wanategemea kazi hiyo kama
ajira yao ya kila siku katika kujiingizia kipato.
"Ukitaka kukamua jipu huwezi kulikanda. Lazima ukamue usaha wote utoke,
na ndiyo pona ya mgonjwa... ajali nyingi, wengi hawajui sheria na
hawataki kujifunza. Lazima tuchukue hatua mapema vinginevyo idadi ya
walemavu itaongezeka siku hadi siku," anasema.
CHANZO: NIPASHE
on Tuesday, November 4, 2014
Post a Comment