Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman
MAHAKAMA
inaangalia uwezekano wa kuruhusu vyombo vya habari kurekodi picha na
sauti kuwezesha vituo vya radio na televisheni kuripoti habari za
mahakama wakati kesi zinaendelea.
Jaji
Mkuu, Mohamed Chande Othman alisema jana mahakama inajifunza kutoka kwa
nchi zinazoruhusu vituo vya redio na televisheni kurekodi na kuripoti
habari wakati kesi zinaendelea.
Alisema
hayo alipozungumza na waandishi wa habari jana wakati wa mkutano baina
ya Baraza la Vyombo vya Habari na Mahakama uliofanyika jijini Dar es
Salaam.
Alisema
utaratibu huo utaanza kwa kuripoti kesi za madai zenye mvuto kwa jamii
na kwamba utaratibu mzima unapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa baada ya
mahakama na vyombo vya habari kukaa pamoja na kujadiliana juu ya
maadili, uhuru na mipaka ya mhimili wa mahakama na vyombo vya habari ili
kuondoa migongano katika kuandika na kuripoti habari za mahakama kwa
kutumia teknolojia ya kisasa.
Hivi sasa waandishi wa habari hawaruhusiwi kupiga picha za video wala kurekodi sauti wakati kesi zikiendelea.
Badala
yake, wanaruhusiwa kuandika habari hizo kisha kuripoti kile
walichoandika bila kuonesha mwenendo mzima wa kesi kwa kutumia sauti na
picha za video.
Jaji
Othman alifafanua kuwa ni lazima mahakama na vyombo vya habari kuweka
utaratibu wa kuripoti kesi kwa kurusha sauti na picha bila kuvuruga
mwenendo wa kesi kwa kukiuka haki hasa za washitakiwa, waathirika na
mashahidi kwa kuwa wote wanahitaji haki sawa katika kupata ulinzi na
hifadhi kulinda utu wao.
“Mfano
sio haki kuwaonesha hadharani waathirika wa kesi ya ubakaji, pia
mshitakiwa yeyote hawezi kuitwa mwizi au muuaji hadi mwisho wa kesi
ambapo mahakama inazingatia ushahidi na kutoa hukumu,” alisema.
Aliendelea
kusema, “Ukitangaza kuwa mtu ni mwizi kabla ya hukumu, ni kumkosea haki
kisheria hivyo ni lazima tuangalie yote hayo kabla ya kuruhusu
utaratibu wa kunakili sauti na picha wakati kesi zinaendelea.”
Jaji
alitoa maelezo hayo wakati wa kuzungumzia mapendekezo yaliyotolewa na
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga
ambaye alisema ili kuboresha uhusiano wa vyombo vya habari na mahakama,
mahakama inapaswa kuwa na msemaji.
Mukajanga
alipendekeza pia mahakama kuandaa taarifa kwa kutumia sauti na picha za
video kuhusu mwenendo wa kesi, kutoa mwongozo wa kutumia simu za
viganjani na vifaa vingine vya mawasiliano kwa njia ya digitali.
Baraza
hilo la kihistoria kati ya mhimili wa Mahakama na vyombo vya habari,
limeazimia kuimarisha ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja kwa
kuheshimu uhuru na mipaka ya kila mmoja na kuzingatia kuwa wote
wanafanya kazi ya kutetea haki za wananchi na wote wamekuwa kimbilio la
wanyonge.HABARILEO
Post a Comment