Aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi katika
Bunge Maalum la Katiba (BMK) Andrew Chenge akitoka katika ukumbi wa
Karimjee jijini Dar es Salaam leo.
ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Kamati ya
Uandishi katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) Andrew Chenge amekataa
kuhojiwa mbele ya Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma
juu ya tuhuma za kunufaika na fedha zilizotoka katika akaunti ya Tegeta
Escrow, wakati alipoitika wito katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es
Salaam leo.
Chenge alitajwa kuwa mmoja wa watu waliopewa fedha na Mkurugenzi wa
kampuni ya PAP, James Rugemalila, zilizotolewa katika akaunti hiyo ya
umma ambayo ilikuwa ikihifadhi hela za Tanesco na IPTL, kiasi cha
shilingi bilioni 1.6, kitendo kilichosababisha kuondolewa katika nafasi
ya Uenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Lakini baada ya kufika mbele ya kikao cha Baraza hilo, kilichokuwa
chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, Chenge alisema
hawezi kuhojiwa na kikao hicho kwa vile suala lake tayari lipo
mahakamani, kauli iliyomfanya Msumi na wajumbe Selina Wambura na Hilda
Gondwe kukosa la kufanya.
Baadaye Jaji Msumi aliwaambia waandishi wa habari kuwa atatoa tamko
la Baraza kuhusu suala hilo kesho, huku likijiandaa pia kuwaita na
kuwahoji wanasiasa wengine, akiwemo Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye naye alipewa kiasi
kama hicho cha fedha.
Wengine watakaoitwa kuhojiwa ni pamoja na mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja, Mkuu wa wilaya ya Korogwe, Mrisho Gumbo na kiongozi
mwandamizi wa Ikulu, anayetajwa kwa jina la Shaaban Gurumo.
(HABARI: DENIS MTIMA, HARUNI SANCHAWA/GPL)
Post a Comment