KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amenusurika kuuawa na mlinzi wake.
Hilo limebainika baada ya kitengo cha ulinzi cha chama hicho kutibua
mpango unaodaiwa kuratibiwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa
(TIS), wa kumuua kiongozi huyo kwa kumtumia mlinzi wake binafsi (PSU),
Khalidi Kagenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa
Kamati Kuu ya chama hicho, Mabere Marando, alisema Kagenzi akiwa mlinzi
binafsi wa Dk. Slaa katika kipindi cha miaka miwili, amebainika kutumiwa
na vyombo vya usalama vya nchi pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kuvujisha siri za chama hicho, na kupewa kazi ya kumuua katibu huyo wa
Chadema.
Akielezea tukio lililombaini mlinzi huyo, Marando alisema lilitokea
Ijumaa iliyopita baada ya mashushushu wa chama hicho kumwona mlinzi huyo
akipanda gari lenye namba za usajili T 213 ARS linalodaiwa kutumiwa na
Ofisa Usalama wa Taifa wa Kinondoni.
“Baada ya kuonekana ndipo mashushu wa Chadema walichukua jukumu la
kumkamata na kumfanyia mahojiano ambapo walifanikiwa kumpekua katika
simu zake mbili zinazotumia mitandao ya Vodacom, Airtel na Tigo.
“Katika simu hizo, walikuta ujumbe mfupi wa maneno uliokuwa ukitoka kwa
…, aliyempigia mara tatu na kumtumia fedha kati ya Desemba 4, mwaka jana
na Julai 14, 2014. Namba nyingine zilizokutwa zilikuwa za maofisa
Usalama wa Taifa,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya upekuzi huo katika ‘Note book’ na simu zake,
waligundua kuwa kigogo mmoja wa ngazi za juu wa CCM alimtumia muda wa
maongezi wa Sh 50,000 kwa namba ya simu 0764 …222 Julai 14, 2014 na
Desemba 4, 2014 alimtumia Sh 150,000.
Marando alisema katika upekuzi wa kwenye simu, walibaini mazungumzo yake
yote yalikuwa yakitumia muda usiopungua saa mbili hadi tatu, na mara
zote ni wakati ambao Chadema walikuwa wakifanya mikutano yao ya ndani.
“Alikuwa akitumia simu yake kurekodi kila kilichokuwa kikizungumzwa
kwenye mikutano yetu na kusambaza kwa CCM, na iligundulika akiwasiliana
na maofisa wa Usalama wa Taifa waliofikia 22,” alisema.
Marando aliongeza kwa kusema kuwa kama isingekuwa suala la kutolewa kwa
uhai wa Dk. Slaa, wasingezungumzia suala hilo na pia anazungumziwa
huenda akachaguliwa kuwa mgombea wa urais wa Ukawa.
Alisema kuwa jana chama hicho kimetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili
kuchukua hatua za kisheria ambao ndio wanaweza kutaja majina ya maofisa
usalama wa waliohusika na mpango huo.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu afya ya Dk. Slaa,
alisema hadi jana alikuwa salama ingawa bado hajapima kubaini hilo.
Marando alisema baada ya kugundulika kufanya hujuma hizo, Ijumaa
iliyopita walimsimamisha majukumu yake ya kumlinda kiongozi huyo hadi
pale uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.
Ingawa chama hicho hakikueleza kiasi cha fedha ambacho mtuhumiwa alipewa
kufanyia shughuli hiyo, lakini kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa kwa
Idara ya Ulinzi wa chama hicho, alionyesha ndani ya simu yake kiasi cha
Sh milioni 7 ambazo zilikuwa muda wa maongezi kwa muda wa miaka miwili.
Alipotafutwa kigogo wa CCM aliyetajwa, hakupatikana ofisini
kwake Lumumba wala Dodoma, na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi
iliita bila kupokewa.
Pamoja na jitihada hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ‘SMS’ hakuweza .
Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kuwa tangu Ijumaa baada ya
kugundulika kwa mpango huo walinzi wa chama hicho walikuwa wakimsulubu
kwa kipigo Kagenzi ili kuweza kupata ukweli.
Huku akiwa anapigwa, Kagenzi alilazimika kutaja majina ya watu wote
waliokuwa wakifanya kazi hiyo ikiwamo kuandika taarifa maalumu ikiwamo
shughuli binafsi za Dk. Slaa.
Polisi Wazungumza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camillus Wambura,
alithibitisha kufikishwa mtuhumiwa huyo katika Kituo cha Polisi
Oysterbay ambapo alisema wanaendelea na mahojiano naye ili kujua ukweli
wa tuhuma zinazomkabili.
“Tumempokea leo (jana) mtuhumiwa, tumeanza kuwahoji waliomleta na
baadaye kumhoji muhusika ili tuweze kubaini ukweli kuhusu tuhuma dhidi
yake,” alisema Kamanda Wambura.
Post a Comment