Mahakama
kuu ya Tanzania katika kikao chake kilichofanyika mkoani Geita imewatia
hatiani na kuwahukumu kunyogwa mpaka kufa, watuhumiwa wa nne wa mauaji
ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi Zawadi Magindu aliyeuwawa mwaka 2008
katika kijiji cha Nyamalulu wilayani.
Kwa kuzingatia ushahidi na utetezi wa pande zote jaji Joaquine
De-mello amesema mahakama imejiridhisha pasipo kuacha shaka yoyote kuwa
watuhumiwa wote wanne walihusika na mauaji ya Bi Zawadi Magindu katika
kijiji cha Nyamalulu wilayani Geita mnamo tarehe 11 mwezi wa tatu mwaka
2008 usiku.
Kwa mujibu wa mashahidi waliojitokeza inasemekana mtuhumiwa namba
mbili Ndahanya Lumola na mtuhiwa namba tatu Singu Siantemi ndio
waliohusika na upimaji wa mifupa ya marehemu Zawadi ambapo hutumia wembe
na shilingi moja kuweka karibu na mifupa ya Albino ili kujua kama
itavuta kama sumaku na kipimo kingine ni redio ambayo huiweka karibu na
mifupa na ikizimika ndio mifupa hiyo huonekana kuwa na ubora tofauti na
hapo mifupa hiyo huwa haifai na hutupwa.
Mashahidi hao wamesema vipimo hivyo havina uhalisia wa aina yoyote kwani hakuna binadamu mwenye mifupa inayokuwa na sumaku.
Aidha jaji De-mello amesema anashangazwa na kesi zote alizosimamia
zinazohusu mauaji ya Albino watuhumiwa wote wanaofikishwa mahakamani ni
wakataji wa mapanga na kuhoji wakataji hao wanapeleka wapi mifupa hiyo?
Na kuwataka wahusika kuhakikisha wanawapata wanunuzi na watumiaji wa
viongo hivyo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Watu waliokutwa na hatia ya kufanya mauaji hayo ni Masalu Kahindi,
Ndahanya Lumola, Singu Siyantemi na Nassoro Saidi ambaye ni mume wa
marehemu Zawadi.
Kwa upande wao watu wenye ulemavu wa ngozi wameipongeza mahakama
kwa kutoa hukumu ya haki inayoashiria kuwapa ulinzi jamii hiyo ya
maalbino.
Post a Comment