CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kimeanza kulisaka Jimbo la Moshi Mjini kwa kutumia helikopta (chopa) ili kiweze kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu ujao.
Katika mkutano wao wa hadhara uliofanyika jana kwenye Viwanja vya Soko la Pasua, Kata ya Bomambuzi, kada wa chama hicho Buni Ramole kwa jina maarufu 'Buni', alitumia usafiri huo kufika eneo la mkutano.
Akihutubia mamia ya wanachama wa CCM na wananchi walioshiriki mkutano huo, Ramole alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepoteza sifa ya kuendelea kuliongoza jimbo hilo hivyo kinapaswa kukaa pembeni.
Alisema umefika wakati wa CCM kuliongoza jimbo hilo ili kuwaletea wananchi maendeleo baada ya jimbo hilo kushikiliwana mbunge wa CHADEMA kwa vipindi vitatu mfululizo.
"Naomba niwaeleze kuwa, jimbo hili kuongozwa na mbunge wa CHADEMA, Bw. Philemon Ndesamburo kwa vipindi vitatumfululizo...katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu lazima lirudi CCM, upinzani hawajafanya kitu zaidi ya kusababisha mateso kwa wananchi, sasa watupishe," alisema.
Aliongeza kuwa, mwaka 2010 wakati Bw. Ndesamburo alikupata ridhaa ya wananchi aweze kuliongoza jimbo hilo kwa awamu ya tatu, aliahidi mambo mengi.
Mambo hayo ni pamoja na kufungua viwanda vilivyofungwa katika Mji wa Moshi lakini hadi sasa ameshindwa kuitekeleza ahadi hiyo hivyo ni wazi kuwa aliwadanganya wananchi.
Kada huyo ambaye pia ni mfanyabiashara, alisema CCM kimejipanga vizuri kuhakikisha kinalichukua jimbo hilo kwa ushindi wa kishindo ambapo moja ya mambo ambayo chama hicho kitafanya baada ya kushinda ni kuwaletea wananchi maendeleo na kufungua viwanda vyote vilivyofungwa.
"Jambo lingine ambalo tutalifanya ni kata zote za Mji wa Moshi, kuunganishwa na barabara za viwango vya lami,nitashirikiana na watendaji wa chama changu kuhakikisha tunapata ushindi wa kishindo...tutaendelea kutumia chopana kupita kila kata ili tuweze kuwafikia wananchi wote ili kuwaeleza ahadi zetu," alisema.
Akizungumzia hatua ya Bw. Ndesamburo kutangaza kutogombea tena ubunge wa jimbo hilo na nafasi hiyo kumpa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Bw. Japhary Michael, alisema inaonesha kuwa CHADEMA hakina demokrasia.
"Hivi karibuni Ndesamburo alitangaza kuachia ubunge na kumkabidhi mikoba yake Japhary Michael, hii inaonyesha wazi kuwa chama hicho hakina demokrasia bali ni sawa na SACCOSya mtu anayeweza kuitumia atakavyo," alisema.
Ramole ni mmoja wa makada wa CCM ambaye ametangaza nia ya kutaka kuwania ubunge wa jimbo hilo muda ukifika.
Mwaka 2010, Ramole alikuwa mmoja kati ya wagombea tisa ndani ya CCM waliojitokeza kuwania ubunge wa jimbo hilo ambapo baada ya kupigiwa kura, alishinda na kushika nafasi ya kwanza akipata kura 1,554.
Nafasi ya pili ilishikwa na Bw. Thomas Ngawaiya aliyepata kura 1,539 ambapo Justine Salakana alishika nafasi ya tatubaada ya kupata kura 1,152.
Licha ya Ramole kuongoza katika kura ya maoni, jina lake lilienguliwa na chama hicho ambapo Salakana aliyeshika nafasi ya tatu, ndiye aliyepeperusha bendera ya chama hicho kwa tiketi ya CCM lakini hakufurukuta kwa Bw. Ndessamburo.
Post a Comment